kwangila

Just another WordPress.com weblog

MISHAHARA YA WABUNGE KENYA: WIZI! WIZI! WIZI!

 

Uingereza  ni mojawepo ya nchi zenye utajiri mkubwa duniani. Katika mwaka wa 2005, nchi hii ilikuwa na GDP pakapita ya $30,900. Yaani ukigawa pato la nchi kwa idadi yote ya wananchi mwakani 2005.  Katika vipimo hivi
Kenya ni mojawepo ya nchi maskini zaidi ulimwenguni. Katika mwaka wa 2005 GDP pakapita ya Kenya ilkuwa $1,200.

Uingereza inamlipa Waziri wake mkuu Ksh milioni 22 kila mwaka.
Kenya inamlipa Mkurungenzi wa Ufisadi nchini Ksh Milioni 30 kila mwaka. Rais Kibaki naye anapata Ksh milioni 24 kila mwaka. Aidha rais Kibaki anapata mshahara mkubwa zaidi ya Waziri mkuu wa Uingereza kwa shilingi Ksh milioni 2 kila mwaka.

Mawaziri nchini Kenya, manibu wao, wabunge ni mojawepo ya watu wanaopokea mishahara ya juu zaidi ulimwenguni kote. Haya yanaendelea wakati ambapo tunawapigia magoti Ungereza na wafadhili wengine kutupa mikopo. Zaidi ya hayo raia wanakufa kwa ajili ya ukame na janga la ukimwi.

Watu hasa wanaostahili nyongeza hii ni walimu, madaktari, waugzi, wafanyikazi wa serikali, ambao hupata mapeni tu baada ya kulala barabarani wakidai nyongeza ya mishahara. Aidha hawa wabunge walafi kama fisi wana huduma nyinginezo nyingi ambazo wanazipokea. Wana pensheni bora zaidi ulimwenguni, huduma za matibabu, bima na marupurupu ya kujinunulia magari ya kifahari.  Isitoshe ni nadra sana kwa hawa kulipa ushuru. Abdulahi ambaye mifugo wake wafa njaa na Musyoki ambaye wanawe wafa njaa ndio wanatozwa ushuru unaowalipa hawa fisi.

Ukitaka kujua ushetani wa mambo haya, tazama tabia zao mjadala unaporushwa hewani kuhusu nyongeza yao ya mishahara.  Raila atakuwa rafikye Kibaki, Ruto ataongea vizuri na Karua. Swala la pesa linawaleta pamoja na wanaliunga mkono pasi Tuju au Balala kukenua kinywa.  Mishahara inapotajwa hamna, ODM , NARC, au CHAMA cha MAPINDUZI.  Wote wanakuwa mapaka wakati huu waking’ang’ania paketi ya maziwa.

Nchini Marekani vuguvugu la kisiasa kwa jina Boston Tea Party, lilipelekea wafanyibiashara, na raia kuandamana kwa ajili ya kile walichokiita ‘utozwaji ushuru kulipa huduma zisizokuwepo’. Kwa mkabala huo, Uingereza ilipokuwa mkoloni wa ulimwengu iliwatoza wakoloniwa ushuru pasi kuwashirikisha abadan kataan katika kutoa maamuzi. 

  Aidha raia hawangekuwa na chuki endapo nyongeza ya mishahara inandamana na utendaji kazi.  Linalonisikitisha ni kwamba utendaji wa wengi wa wabunge hawa ni butu. Kazi yao ni kupinga miradi ya kufaidi raia ili waweze kuwa na silaha ya kushambulia serikali na kurudi bunge baada ya miaka mitano. Kwa sababu wameonyesha kwamba nia yao ni kuvuna kadri ya uwezo wao ni dhahiri kwamba hawa wenye matumbo makubwa hawako tayari kuhudumia raia. Hawafai kamwe kuwa ndio wanajiwekea kiwango cha mshahara na kutuwekea kiwango cha ushuru tunachostahili kulipa.

Iwapo hakimu Aaron Ringeera angekuwa amewatia baadhi ya hawa jela angalau tungesema anastahili kulipwa nusu ya mshahara wake bali sio milioni 30 kwa mwaka. Lakini bwana huyu mtoka Meru ameishia kuwatia korokoroni wauzaji sukumawiki na waoshaji vyoo eti kwa sababu hawajalipa ushuru na kamwe hatawagusa wabunge na mawaziri. Si eti hamna ushahidi wa kuwatia vizuizini wabunge. Ripoti za Mhasibu mkuu na kamati za bunge zimetoa mapendekezo ya baadhi ya wabunge hawa kuhukumiwa ‘kifo’ kwa ufisadi wanaouendeleza. Kwa misingi hii basi Ringeera anakuwa fahali asoweza kutungisha mamba; Simba kibogoyo anayewinda nzi badala ya nyati.

Nina uhakika hamna mbunge hata mmoja anayewatetea maskini. Wanaojaribu wanacheza siasa ili waonekane wanajinasibisha na maskini lakini wapi. Kalonzo juzi amesema nyongeza ya mishahara haifai sasa. Je umemsikia akisema kwamba nyongeza aliyopewa ataitoa kwa akina Wambua wenye njaa huko Mwingi Kaskazini? 

Wapigaji kura tunastahili kukataa tabia hii maradufu kabla ya nchi kutangazwa haina pesa zozote. Tuamke zaidi ya vile tuliamka tulipokataa katiba tupiganie usambazaji sawa wa utajiri wan nchi. Ukweli ni kwamba hamna mbunge(awe katika serikali au upinzani) atakayetuunga mkono katika vita hivi maanake tunajaribu kupunguza kiasi cha ugali katika sahani zao. Tutafanikiwa kwa kuokota sahihi za raia wanaopinga nyongeza ya mishahara. Tukishapata mamilioni ya sahihi tuwapelekee wabunge pia watie sahihi. Atakayekataa, tumwondoe katika orodha ya wagombea 2007. Baada ya hapo tutumie kipengele hiki kuwageza wagombea wa Urais. Akina Raila, Kibaki , Kalonzo, Balala na wengine wanastahili kuchaguliwa endapo watakubali kupunguza mishaharayao na ya wabunge wenzao. Anayekataa aondolewe katika orodha ya wagombe wa Urais.

Tukishapata M/Wagombea wa Urais, tulazimishe kuunda kwa kamati isokuwa na mbunge yeyote itakayotathmini mishahara ya wabunge.Baada ya kamati kuundwa tulazimu, wabunge kulipa ushuru pia. Sote Wakenya twenda msalani. Hakuna wakudai kwamba kinyesi chake ni cha dhahabu. Hivyo kila mmoja anastahili kulipa ushuru. Huu ndio utakuwa mkataba wetu na serikali ijayo.     

 
Advertisements

May 2, 2006 - Posted by | Uncategorized

6 Comments »

 1. halafu,sivyo nilivyoudhika kusoma ati Kibaki kaongeza watu misharaha siku ya wafanyikazi kwa asilimia ya upuzi kabisa. Ukitafakari mahela wanayokusanya wabunge hawa hutatarajia kamwe raisi mzima wa taifa kufungua kinywa na kudai nyongeza toka elfu 4 na vijimia kidogo hadi alfu tano.Ubinafsi ulioje huu….

  Comment by wawuda | May 3, 2006 | Reply

 2. Hivi wizi wa wabunge wa Kenya utaisha lini? Hivi hawa hawatambbui wanatuletea kero hata sisi kwenye nchi zetu ambazo kuna watu wanatamani kuiga tabia hii mbaya ya kutu? Nini nafasi ya wananchi wa Kenya baada ya kuisha MAU mAU HAKUNA HAJA YA KUANZAISHA NYINGINE KUPAMBANA NA WAZUNGU HAWA WEUSI?

  Comment by bONIPHACE mAKENE | May 12, 2006 | Reply

 3. Halafu tunaambiwa kuwa kenya ni nchi masikini! Masikini kivipi wakati viongozi wake ni wafalme na malikia? Wezi watupu!

  Comment by ndesanjo | May 14, 2006 | Reply

 4. Halafu waingereza wanawapa msaada unaojadiliwa na mawaziri wa wanaolipwa kidogo kuliko mawaziri wa Kenya. Hivi huo msaada au biashara?????

  Comment by Indya | May 23, 2006 | Reply

 5. Hapa marekani, maswala muhimu (kwa mfano kuongeza ushuru wa mji, kukomesha uvutaji wa sigara katika maeneo fulani na kadhalika) huwa yanapigiwa kura wakati wa uchaguzi. Je, yawezekana pia Wakenya wafanye hivyo kuhusu mishahara ya waheshimiwa(???) wetu?

  Comment by Mimi | December 22, 2006 | Reply

 6. ulafi ulioje! kenya tuaishi kama wafungwa. tangu lini mzalendo wa kenya, mzaliwa kenya hakawa mfungwa na mtumwa? mafisi hawa hawatosheki na walicho nacho ili hali watu wa mandela na sehemu zingine nchini wanan kufa njaa! wakenya si wazalendo tuabaki vinywa wazi bila ya kusema. washindwe na washindwe kabisa.

  Comment by waednya | August 9, 2007 | Reply


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: