kwangila

Just another WordPress.com weblog

WIZARA YA NCHI ZA KIGENI AFRIKA MASHARIKI.

Nchi zilizoendelea zimejua kutambua vipawa vya wanasiasa wakiwa wangali vijana. Katika hali hii kipawa cha mwanasiasa kinapotambulika, yeye huwekwa katika mazingira ambamo yatamsaidia kukuza kipawa kile ili labda siku za usoni aweze kufaidi nchi akiwa na tajriba toshelevu. Nchini Marekani kwa mfano, chama cha upinzani kimetambua kipawa cha Barrack Obama; na inasemekana kwamba licha ya yeye kuwa Mmarekani mweusi, ana nafasi nzuri hata ya kuwania Urais siku za usoni. Hivyo basi ,amekuwa malighafi ya kutegemewa katika kuzua na kutetea mijadala inayofaidi umma kwa jumla. 

Katika kanda ya Afrika Mashariki , Wizara ya Nchi za Kigeni huwa na mchango si haba katika kukuza matamanio ya mbunge ya kuongoza nchi wakati mmoja. Tom Mboya alijengwa vyema na Wizara hii kiasi cha kuonekana kuwa bora zaidi kumliko Rais mwenyewe Kitaifa na kimataifa. Kalonzo Musyoka alipoteuliwa kuwa Waziri katika wizara hii, ilimsaidia pakubwa kujijenga Kitaifa na Kimataifa kiasi kwamba hata serikali za mpito za Somalia naSudan zingali zinakumbuka juhudi zake za kuleta amani katika nchi hizi mbili. Si ajabu kutambua kwamba hii ndiyo sababu imempelekea kuwa na matamanio ya kuwania Urais ijapo 2007.  

  Nchini Tanzania, Jakaya Kikwete amekuwa Waziri wa nchi za kigeni kwa miaka 10 sasa. Kipindi hiki kilimpa nafasi ya kutambua ulimwengu tajriba ambayo ni muhimu kwa rais yeyote barani Afriika. Haikosi zaidi ya 80% ya Watanzania wamempa kura kuiongoza bongo.   Hii ina maana gani? Marais waliopo katika kanda ya Afrika Mashariki wanastahili kutambua siri hii. Kwamba tunawahitaji wao Wateue watu ambao wana uwezo wa kuwa Marais katika Wizara za nchi za Kigeni. Kwa njia hii, watawapa nafasi ya kutangamana na mataifa mengine ;tajriba ambayo itakuwa muhimu sana kwao endapo watakuwa Marais siku za usoni. Waziri kama huyu hastahili kuajiriwa leo na kufutwa kazi kesho kama ilivyo nchini Kenya. Hii ni kwa sababu huyu ndiye Afisa wa Uhusiano bora kati ya taifa na Ulimwengu kijumla. Haifurahishi kamwe kusikia kwamba leo Chirau Mwakere ametoa hotuba Marekani kama Waziri wa Nchi za Kigeni kish Kesho Raphael Tuju ndiye Waziri mpya wa nchi za kigeni.   Rais alioko mamlakani anastahili kumteua mtu msomi, anayependeka na wengi nchini kwa ajili ya kuzua sera na kuzitetea kitaifa na kimataifa. Sera zinazolenga kukwamua nchi kutokana na umaskini, sera zinazokweza nchi katika kiwango cha kimataifa. Waziri huyu anastahili kuwa msemaji hodari. Aielewe lugha ya Kiswahili, Kiingereza na lugha zingine za kimataifa. Awe mtu anayeielewa mifumo ya kiuchumi na sheria za kimataifa. Huyu ni mtu asiyestahili kuwa na mtazamo finyu wa maisha. Hastahili kuwa Mkabila na juhudi zake ndizo zinastahili kumzolea sifa kitaifa na katika ngazi za kimataifa.Hivyo basi Marais wa Kanda ya Afrika Mashariki hawastahili kuongozwa na ubinafsi katika kuwateua Mawaziri wa nchi za kigeni na wala hawastahili kuwaona waliwateua kama washindani katika kuwania Urais siku za usoni. Kwa njia hii, Rais atakuwa anajali maslahi ya nchi siku za usoni japo huenda yachukue muda.    Katika kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwajenga Marais wa siku zijazo. Licha kwamba Jakaya Kikwete alikuwa na nia ya kugombea Urais kitambo sana, haikumpelekea Rais Benjamin Mkapa kumwachisha kazi. Aidha sababu ya nyota ya Kikwete kung'aa wakati wa kampeni dhidi ya ile ya wapinzani wake ni kutokana na tajriba ya miaka 10 aliyoipata katika Wizara ya Nchi za Kigeni. Isitoshe Mkapa alijitokeza wazi kumuunga mkono Waziri wake tofauti na Rais mstaafu Daniel Moi aliyeamua kumuunga mkono kijana machachari badala ya aliyekuwa Waziri wa nchi za kigeni Mheshimiwa Kalonzo Musyoka.  Nchi ya Kenya kwa maoni yangu inakosa uhusiano mwema na jamii ya Kimataifa kutokana na kuyumbayumba kwa Wizara ya nchi za Kigeni. Licha ya Chirau Mwakwere kushtakiwa kuwa na uhusiano wa mahawara jijini Nairobi, Rais Kibaki alimteua Waziri wa nchi za kigeni na kumhamisha Kalonzo Musyoka. Kabla ya ubwabwa kumtoka Mwakwere shingoni amehamishwa na akateuliwa Raphael Tuju.     Raphael Tuju ni msemaji hodari; ndio sikatai. Ana elimu hasa tunapoelezwa kwamba aliisomea taaluma ya habari na ni Alumunae wa shule maarufu nchini ya Starehe. Kasoro yake ni kwamba Wakenya walio wengi wanamhusisha na vifo vilivyotokea Mkoani Nyanza. Hali ambayo inamfanya asipendeke hasa miongoni mwa jamii ya Waluo. Ana uwezo wa kuwa Waziri katika Wizara yoyote ile lakini si hii ya kumwakilisha Rais katika nchi za kigeni. Swali ni je Tuju akipewa miaka mingine 5 kama Waziri wa nchi za kigeni atakuwa na umaarufu na uwezo wa kuomba kura na kupewa na Wakenya walio wengi?    

Advertisements

March 27, 2006 - Posted by | Uncategorized

2 Comments »

 1. Karibu David wewe ulikuwa mmiliki wa Gazeti Tando tangu mapema ila ulichelewa. Hata hivyto umeingia kwa kasi sana na vitu vingi vikali. Nitakuwa napita hapa kunywa kahawa.

  Comment by Boniphace Makene | March 27, 2006 | Reply

 2. Mheshimiwa Maithya, mimi nafurahi sana kama Mkenya mtetea Kiswahili kuona kwamba kunao Wakenya wenzangu ambao hawana ile taasubi ambayo imeenea hapa nchini kama yale mablanketi yenye viini vya ugonjwa wa ndui ambayo yalisambaziwa Wamarekani asilia na serikali yetu tunayoiiga na kuikubalia kutuendesha tete katika mambo ya demokrasia na uongozi bora, ucha Mungu (Kumbuka kauli ya Tunamtumainia Mungu kwenye hela)-lakini tuache hilo gumzo kwani ni lenye kujaza tama na kuchosha taya kiasi. Niseme kwamba ni furaha kukuona Mkenya unayeweka kifua mbele kimataifa kwa kujieleza kwa Kiswahili.

  Pili niseme kwamba, kama unataraji kwamba mfumo wetu wa kisiasa na mazoea tuliyo nayo ni ya watu kujengana na kutayarishana kwa ajili ya taifa, basi nafikiri wewe ni mgeni katika eneo hili la sayari hii.Kama unafikiri kwamba watawala wetu wana haja yoyote ya kutukwamua kutoka katika kitu chochote ambacho si matumaini yetu ya pepo, basi matarajio yako ni makubwa kupindukia na utavunjika roho kila mara. Ukiangalia mfumo wa utawala huku kwetu Kenya, ni wa kujenga jeta la rais na nyangumi wa mawaziri na vigogo serikalini. Chukua mfano wa rais Moi ambaye alitutawala kwa muda mrefu zaidi. Alipoichukua sifa ya ‘Mtukufu Rais’, ilikuwa ni kosa la uhaini kufikiri kwamba kungelikuwepo wakati mmoja ambao angalikuwa hayuko mamlakani. Kumbuka kwamba hata kifungo cha sheria kililetwa bungeni na kupitishwa kuwa sheria kwamba ilikuwa ni hatia kufikiria, kuota….kuhusu kifo cha rais, au kutokuwepo kwake mamlakani. Ndiposa tukawa na visa vingi sana vya watu kuteswa kwenye majumba mbali mbali ambayo yalitapakaa kote nchini.

  Kimsingi ni kwamba, Watanzania walikuwa na bahati nzuri sana ya kuongozwa na mzalendo Mwalimu Nyerere. Wakati ambapo Nyerere alijenga uzalendo na utaifa, mwenzake Kenyatta alijenga ukabila. Umetoa mfano wa Mboya kama waziri wa mambo ya kigeni. Ni kwa nini akapigwa risasi na kuuawa? Kwa sababu umaarufu wake ulikuwa wa kiasi cha kumfanya kuwa rais, ila tu hakutoka katika kabila la rais wa wakati huo. Sijui ni kwa nini hukumtaja marehemu Robert Ouko ambaye naye kapigwa msumari na kina Moi kwa sababu alikuwa ni nyota. Yule bwana alikuwa na elimu na ushawishi wa kutosha. Inakumbukwa kwamba Joji Kichaka mkubwa alipokuwa uongozini kule kwenye taa nyinigi, kuna hii ziara ambayo ndiyo iliyokuwa safari ya Ouko ya kwenda Kaivari. Inasemekana kwamba Joji Kichaka alikataa kuzungumza na Moi na akachagua kuzungumza naye Ouko. Ole wake waziri wa mambo ya kigeni! Gofu la maiti yake lilipatikana kwenye kilima fulani kule karibu na Koru.

  Marais wa Kenya huwa wanajitayarisha wao wenyewe kutawala milele. Marais wa Tanzania wanafuata nyayo walizoachiwa na Mwalimu. Zilikuwa nyayo za mzalendo halisi. Sisi hadi wa leo tunazifuata nyayo za Kenyatta. Hatujioni kama taifa bali tunajiona kama watu tunaotoka katika sehemu fulani ya nchi na kuzungumza lugha fulani. Hebu mwangalie rais wetu Kibaki! Huwezi kuamini kwamba huyu ni mtu ambaye amewahi kutangamana na jumuiya ya kimataifa. Yeye ni mzee wa Kikikuyu tu. Sasa mtu kama huyu atamtayarisha nani kuchukua madaraka akishaondoka?
  Katika miaka hii minne ambayo maeongoza, tungelikuwa tumeona angalau mwelekeo.

  Mwenzangu Maitha, Watanzania wana historia na uzoefu wa zaidi ya miaka arobaini. Sisi ingawa tutasikika tukijidai tukiwa tumeshika chupa za vinywaji vya kizungu, tukiwa kwenye majumba yenye majina ya kizungu, tukiwa tumevalia nguo zinazomtajirisha na kumtukuza mzungu, tukiongea lugha isiyo yetu, kwa madaha tukisema vile tulivyo mbele katika eneo letu, ninaomba kukubaliwa kufarakana na kutofautiana na maoni na bwabwaja kama hizo. Nawavulia kofia wazalendo wa Tanzania.

  Comment by Amadi kwaa Atsiaya | March 28, 2006 | Reply


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: