kwangila

Just another WordPress.com weblog

WAMAREKANI WANAVYOMTHAMINI MBWA.

 

 

            Tofauti na wakenya walio wengi, kwa Wamarekani mbwa ni almasi iwapo si dhahabu. Huyu ni kiumbe aishiye kwenye makasri na wanadamu huku Marekani. Akiwa ndani ya kasri basi mbwa huyu ana haki ya kuingia chumba chochote atakacho pasi kubisha hodi. Haijalishi chumba atakamoingia mbwa atampata mwenye nyumba akiwa uchi au la. Waama mbwa wa kiafrika atamwonea gere mbwa wa kimarekani kwa jinsi ambavyo mbwa huyu analelewa kwa utashi.

            Ni nadra kumpata mkenya akimpa busu mbwa. Wamarekani swala hili si hoja. Nikidhani mwenye mbwa atampa mbwa wake busu la kukata na shoka kuliko jinsi atampa mpenziye. Kwetu sisi hatuwabusu mbwa mbali tunavitupilia mbali vyombo alivyonusanusa mbwa huyu.

            Ukija Marekani ndugu utashuhudia haya bila shaka. Mabwana na mabibi wakiwa ziarani na mbwa wao hawasahau kubeba mikoba ya kuokotea vinyesi vya mbwa. Mwenye mbwa yu macho kutizama mbwa wake atakapochutama. Mara moja atatoka mbio kama mshale kwenda kuokota kinyesi na kukitia mkobani. Eti wanjali mazingira! Kwetu sisi harufu ya kinyesi cha mbwa itaweka makunyugu pua zetu na kutufunga macho kwa ghafla angalau tusikione kinyesi.

            Waama mbwa nchini marekani wana bajeti kubwa yakhe! Nina uhakika kiasi cha fedha kitumiwacho kwa mbwa nchini Marekani kila mwaka chatosha kulikwamua bara la Afrika kutoka katika lindi la umaskini. Mbwa atalishwa kwa chakula kilichosawazishwa, atakingwa kutokana na maradhi, atakuwa na yaya wa kumlinda nyumbani miongoni mwa matilaba mengine.

            Waliotazama janga la kibunga cha Katrina mtakubaliana nami kwamba ilkuwa heri mbwa kuokolewa kwanza kisha tuanze kutafuta binadamu alipo. Mbwa wengi waliokolewa kutoka vyomba vilivyokuwa vimesombwa huku watu wakifa maji.

            Iwapo bwana enda safari na mbwa wake na iwe kwamba atatumia gari basi mbwa atakuwa na kiti chake spesheli. Ole wako mkenya uliozoea kuomba lifti. Samahani maanake kiti kishakaliwa tayari na mbwa! Ukipenda basi jisombe nyuma palipo mizigo na katu usitatize starehe za mbwa wangu. Ikizidi vilevile, usimtamzame mbwa wangu kwa jicho la dharau maanake nitakufungulia mashtaka kortini.

            Visa vingi kortini ni vya huyu kamwiba mbwa wangu, yule alimtisha mbwa wangu, huyo hampendi mbwa wangu n.k. Mbwa ni msamiati wa kila mara bongoni mwa Mahakimu na Viongozi wa mashtaka. Mbwa angekuwa na uwezo wa kujitetea angetiwa vizibani kujitetea huku Marekani.

            Amini usiamini huku Marekani talaka ni jambo la kawaida. Ndoa huku ni kandarasi. Nikichoshwa na yako mapenzi nenda potelea mbali! Uniache na mbwa wangu. Imekuwa heri kwao kuishi na mbwa kuliko kuishi na libaba lililioshiwa na nguvu za kiume. Nadhani mbwa angekuwa na uwezo wa kufanya mapenzi na binadamu basi ungempata vitandani na wake au waume za watu wakizicheza.

                        Mambo yalivyo huku ndugu ni kwamba wamarekani wanampa mbwa nafasi ilyovuka mipaka. Ni sawa siwapingi lakini inapofikia kiwango cha kutojali binadamu mwenzako, mpenzio n.k basi nafikiri huku ni kukengeuka. Jumapili baadhi yao hawendi kumwabudu mwenyezi MUNGU aliyewapa hao mbwa. Badala yake huwa ni nafasi nzuri ya kuwatembeza mbwa wao. Mambo Mbotela, unambie leo, huu ni uungwana?

Advertisements

March 27, 2006 - Posted by | Uncategorized

No comments yet.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: