kwangila

Just another WordPress.com weblog

MAREKANI INAVYOFADHILI VITA BARANI AFRIKA.

Habari kwamba Marekani inawafadhili mibabe wa vita nchini Somalia inastahili kuwaamsha viongozi wa bara la Afrika na ulimwengu kwa jumla. Tangu 1992 hakujakuweko serikali nchini Somalia baada ya nchi hiyo kusombwa na mizozo ya kikabila. Serikali ya Siyad Barre ililazimika kung'atuka baada ya baadhi ya mibabe wa kivita kuziongoza jamii zao dhidi ya serikali. Hali hii ilipelekea Wasomali wengi kukikimbilia nchini Kenya. Hivi sasa kuna zaidi ya Wakimbizi 100,000 katika kambi ya Wakimbizi ya Daadab Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Ni muhimu kutaja kwamba katika zile harakati za vita vya  kikabila, Wasomali wengi waliuawa, wengine kubakwa , wengine walitafunwa na wanyama pori na zaidi wengine wamekuwa walemavu wa kudumu.

Katika mwaka wa 2004 serikali ya mpito iliundwa rais wake akiwa Rais Abdullahi Yusuf. Haya yote yalifanyikia Nairobi maanake pilipili ilikuwa imetapakaa kote mjini Mogadishu na miji mingine. Hata hivyo ilibidi Serikali ya Adullahi kuhamishwa hadi mji salama kiasi wa Johar nchini Somalia baada ya shinikizo kutoka jamii ya kimataifa. Serikali hii haingeweza kupata makazi Mogadishu maanake mibabe wa vita wenye silaha kali wangali wanathibiti kila kitu jijini Mogadishu. Asilimia kubwa ya serikali hii ya Abdullahi ni mibabe wa kivita ambao ni sugu hata hivi leo. Hawakubaliani kwa asilimia 100 na sera zinazopitishwa na bunge.

Licha kwamba serikali ipo sasa, Abdullahi amedai kwamba Marekani inawafadhili mibabe wa kivita badala ya kuifadhili serikali kupitia taasisi zinazostahili kutumika. Alisema haya nchini Uswidi na zaidi akasema kwamba Marekani haiko radhi kuona kwamba nchi hii ya Somalia ina amani. Aidha ufadhili wanaopata mibabe hawa unawapelekea kuwa sugu zaidi kiasi kwamba hawasikii lolote analosema Abdullahi. Hawatambui katu kwamba kuna rais, kazi yao ni kushirikiana na Marekani kuongeza vita nchini Somalia kwa madai eti wanayawinda makundi ya Ki-Alqaida. Bwana wao sasa ni Marekani bali sio Abdullahi.

Mataifa mengine barani Afrika ambayo yamesombwa katika mizozo barani Afrika ni yale yenye mafuta na madini adimu duniani. Mifano ya mataifa haya ni Sudan, Nigeria, Congo, n.k. Nitarejelea Sudan pekee katika mjadala huu. Je Marekani inachangia vipi katika mzozo wa Darfur nchini Sudan?

Eneo la Darfur linajulikana kama lenye mafuta na kwa muda mrefu limekuwa kitega uchumi cha serikali ya Sudan. Marekani haifurahishwi na uamuzi wa serikali ya Sudan kuuzia mafuta mataifa mengine mbali sio Marekani. Marekani ilipotaambua hili, iliamua kumtumia John Garang kuipiga vita serikali. Marekani iliwahami wanajeshi wapinzani wa SPLA na SPLM walioongozwa na John Garang. Swala kuu lilikuwa  Sudan kusini iwe taifa huru. Kwa njia hii Marekani ingeweza kushauriana na serikali ya John Garang (ambaye angekuwa rais wa Sudan Kusini )bila kuomba ruhusa kutoka kwa el-Bashir. Hta hivyo Garang aliaga katika ajali ya ndege pindi tu mkataba ulipotiwa saini jijini Nairobi. Hali hii ilipelekea makamu wake Savar Kiir ambaye hana elimu yoyote kuchukua hatamu za uongozi. Kubuka John Garang alikuwa Daktari kando ya kuwa mwanajeshi.

Katika mifano hii miwili ya Somalia na Sudan, ni wazi kwamba kuwepo mizozo barani Afrika kunafadi Marekani. Wanafaidika na wakimbizi maanake wanawahamisha baadaye hadi nchini Marekani kufanya kazi za kishenzi. Habari nilizopokea hivi juzi ni kwamba Marekani inawahamisha wakimbizi zaidi ya 30,000 kuja Marekani kufanya kazi. Nilidhibitisha haya nilipowazuru Wakimbizi wa Kisomalia ambao wanaishi Providence nchini Marekani. Aliyesema utumwa ulitoweka ungalipo hadi hivi leo hasa katika uhusiano wa Marekani na Mataifa yenye mizozo barani Afrika.

Faida ya pili wanayolenga Wamarekani ni kutokana na kuwepo mizozo ni mafuta kwa ajili ya magari yake, ndege na kupasha vyumba joto wakati wa baridi. Unaposikia Marekani inatafuta mafuta barani Afrika imebeba silaha kwa mkono wa kushoto ili kuwapa wapinzani wa serikali endapo itanyimwa mafuta. Si eti Marekani haina mafuta yake, bali wanahifadhi rasilimali zao kwanza, watumie visima vya ulimwengu kisha  warudie kuchimba vyao visima vya ulimwengu vinapokauka. Hii ndiyo sababu ninashuku kushuka mizozo katika mataifa yanayoipa Marekani leseni ya kuchimba visima nchini mwao. Ni wazi kwamba baada ya mataifa ya mashariki ya kati kutambua ushetani wa Marekani, yameanza kukatiza kiasi cha mafuta yanayokwenda Marekani. Halli hii inapelekea Marekani kuanza kuchimba mafuta barani Afrika. Hii ni dalili ya mizozo zaidi barani Afrika siku za usoni. 

May 9, 2006 Posted by | Uncategorized | 11 Comments

MISHAHARA YA WABUNGE KENYA: WIZI! WIZI! WIZI!

 

Uingereza  ni mojawepo ya nchi zenye utajiri mkubwa duniani. Katika mwaka wa 2005, nchi hii ilikuwa na GDP pakapita ya $30,900. Yaani ukigawa pato la nchi kwa idadi yote ya wananchi mwakani 2005.  Katika vipimo hivi
Kenya ni mojawepo ya nchi maskini zaidi ulimwenguni. Katika mwaka wa 2005 GDP pakapita ya Kenya ilkuwa $1,200.

Uingereza inamlipa Waziri wake mkuu Ksh milioni 22 kila mwaka.
Kenya inamlipa Mkurungenzi wa Ufisadi nchini Ksh Milioni 30 kila mwaka. Rais Kibaki naye anapata Ksh milioni 24 kila mwaka. Aidha rais Kibaki anapata mshahara mkubwa zaidi ya Waziri mkuu wa Uingereza kwa shilingi Ksh milioni 2 kila mwaka.

Mawaziri nchini Kenya, manibu wao, wabunge ni mojawepo ya watu wanaopokea mishahara ya juu zaidi ulimwenguni kote. Haya yanaendelea wakati ambapo tunawapigia magoti Ungereza na wafadhili wengine kutupa mikopo. Zaidi ya hayo raia wanakufa kwa ajili ya ukame na janga la ukimwi.

Watu hasa wanaostahili nyongeza hii ni walimu, madaktari, waugzi, wafanyikazi wa serikali, ambao hupata mapeni tu baada ya kulala barabarani wakidai nyongeza ya mishahara. Aidha hawa wabunge walafi kama fisi wana huduma nyinginezo nyingi ambazo wanazipokea. Wana pensheni bora zaidi ulimwenguni, huduma za matibabu, bima na marupurupu ya kujinunulia magari ya kifahari.  Isitoshe ni nadra sana kwa hawa kulipa ushuru. Abdulahi ambaye mifugo wake wafa njaa na Musyoki ambaye wanawe wafa njaa ndio wanatozwa ushuru unaowalipa hawa fisi.

Ukitaka kujua ushetani wa mambo haya, tazama tabia zao mjadala unaporushwa hewani kuhusu nyongeza yao ya mishahara.  Raila atakuwa rafikye Kibaki, Ruto ataongea vizuri na Karua. Swala la pesa linawaleta pamoja na wanaliunga mkono pasi Tuju au Balala kukenua kinywa.  Mishahara inapotajwa hamna, ODM , NARC, au CHAMA cha MAPINDUZI.  Wote wanakuwa mapaka wakati huu waking’ang’ania paketi ya maziwa.

Nchini Marekani vuguvugu la kisiasa kwa jina Boston Tea Party, lilipelekea wafanyibiashara, na raia kuandamana kwa ajili ya kile walichokiita ‘utozwaji ushuru kulipa huduma zisizokuwepo’. Kwa mkabala huo, Uingereza ilipokuwa mkoloni wa ulimwengu iliwatoza wakoloniwa ushuru pasi kuwashirikisha abadan kataan katika kutoa maamuzi. 

  Aidha raia hawangekuwa na chuki endapo nyongeza ya mishahara inandamana na utendaji kazi.  Linalonisikitisha ni kwamba utendaji wa wengi wa wabunge hawa ni butu. Kazi yao ni kupinga miradi ya kufaidi raia ili waweze kuwa na silaha ya kushambulia serikali na kurudi bunge baada ya miaka mitano. Kwa sababu wameonyesha kwamba nia yao ni kuvuna kadri ya uwezo wao ni dhahiri kwamba hawa wenye matumbo makubwa hawako tayari kuhudumia raia. Hawafai kamwe kuwa ndio wanajiwekea kiwango cha mshahara na kutuwekea kiwango cha ushuru tunachostahili kulipa.

Iwapo hakimu Aaron Ringeera angekuwa amewatia baadhi ya hawa jela angalau tungesema anastahili kulipwa nusu ya mshahara wake bali sio milioni 30 kwa mwaka. Lakini bwana huyu mtoka Meru ameishia kuwatia korokoroni wauzaji sukumawiki na waoshaji vyoo eti kwa sababu hawajalipa ushuru na kamwe hatawagusa wabunge na mawaziri. Si eti hamna ushahidi wa kuwatia vizuizini wabunge. Ripoti za Mhasibu mkuu na kamati za bunge zimetoa mapendekezo ya baadhi ya wabunge hawa kuhukumiwa ‘kifo’ kwa ufisadi wanaouendeleza. Kwa misingi hii basi Ringeera anakuwa fahali asoweza kutungisha mamba; Simba kibogoyo anayewinda nzi badala ya nyati.

Nina uhakika hamna mbunge hata mmoja anayewatetea maskini. Wanaojaribu wanacheza siasa ili waonekane wanajinasibisha na maskini lakini wapi. Kalonzo juzi amesema nyongeza ya mishahara haifai sasa. Je umemsikia akisema kwamba nyongeza aliyopewa ataitoa kwa akina Wambua wenye njaa huko Mwingi Kaskazini? 

Wapigaji kura tunastahili kukataa tabia hii maradufu kabla ya nchi kutangazwa haina pesa zozote. Tuamke zaidi ya vile tuliamka tulipokataa katiba tupiganie usambazaji sawa wa utajiri wan nchi. Ukweli ni kwamba hamna mbunge(awe katika serikali au upinzani) atakayetuunga mkono katika vita hivi maanake tunajaribu kupunguza kiasi cha ugali katika sahani zao. Tutafanikiwa kwa kuokota sahihi za raia wanaopinga nyongeza ya mishahara. Tukishapata mamilioni ya sahihi tuwapelekee wabunge pia watie sahihi. Atakayekataa, tumwondoe katika orodha ya wagombea 2007. Baada ya hapo tutumie kipengele hiki kuwageza wagombea wa Urais. Akina Raila, Kibaki , Kalonzo, Balala na wengine wanastahili kuchaguliwa endapo watakubali kupunguza mishaharayao na ya wabunge wenzao. Anayekataa aondolewe katika orodha ya wagombe wa Urais.

Tukishapata M/Wagombea wa Urais, tulazimishe kuunda kwa kamati isokuwa na mbunge yeyote itakayotathmini mishahara ya wabunge.Baada ya kamati kuundwa tulazimu, wabunge kulipa ushuru pia. Sote Wakenya twenda msalani. Hakuna wakudai kwamba kinyesi chake ni cha dhahabu. Hivyo kila mmoja anastahili kulipa ushuru. Huu ndio utakuwa mkataba wetu na serikali ijayo.     

 

May 2, 2006 Posted by | Uncategorized | 6 Comments

SIKUKUU YA KUVUTA MARIJUANA MAREKANI.

Ilikuwa saa kumi na dakika ishirini tarehe ishirini mwezi wa nne. wanafunzi wa chuo kikuu cha Brown walifurika uwanjani kwa madai eti wanasherehekea majilio ya msimu wa joto. Uwanja mzima ulifurika vimwana na maghulamu weupe wengi na weusi wachache. Kama kawaida kwota sketi zilikuwa nyingi huku baadhi ya mibabe wakiwa kifua wazi kuonyesha malaika zao. Busu zilikuwa si haba. za waume kwa waume, wake kwa wake na zingine za waume kwa wake. Kila mtu alionekana mwenye furaha iliyovuka mipaka. Vicheko havikuwa vya kawaida. Ungefika pale ndugu ungedhani wanafunzi jamani wameanza kupagawa. Wachuuzi wa vyakula walikuwa chonjo kuokota dola. Walijua hii ni siku ambayo wanafunzi hula pasipo kuweka breki.

Hali hii isiyo ya kawaida ilinipelekea kuuliza maswali mbona leo wanafunzi wa chuo kikuu wana furaha isokuwa na kifani? Wanafunzi wangu hawakuachwa nyuma pia bali waliniomba rukhsa ya kujumuika na wenzao. Waliita sikukuu ile 4:20 at 4:20 maanake tarehe ishirini Aprili, saa kumi na dakika ishirini. Kwa kawaida niliwajua Wamarekani kama watu wasokuwa na furaha; watu wanaovalia tabasamu kwa muda unapokutana nao; watu waliojawa na upweke kiasi cha kulala vitandani na mbwa wao; watu wasiojumuika na wenzao kwa urahisi labda kuwe ile waiitayo 'appointment'.

Kulikuwepo harufu aina yake katika uwanja mzima. Kila mmoja alionekana kuvuta kitu fulani chenye muundo wa sigara. Moshi wa kile walichovuta ulipeperushwa na upepo mwororo hadi nilipokuwa. Hapo nikajua kuna jambo linaendelea uwanjani. Harufu hii haikuwa ya kawaida. Nilianza basi kuchanganua matukio na kuyaoanisha. Kicheko na vitendo visivyo vya kawaida uwanjani nilivioanishwa na walichokuwa wakivuta wana wa watu. Nilipokuwa mchanga niliambiwa kwamba mtu anapovuta Marijuana huwa na tabia zisizo za kawaida. Mojawepo ya ngano nilizopashwa ni za mvutaji fulani, aliyepika ugali mkubwa kisha akapika 'kijiugali' kingine kidogo eti kiwe kitoweo cha ugali ule mkubwa.

Lakini iwapo hawa wanavuta marijuana mbona basi polisi wamejaa uwanjani? Sikuamini hadi nilpopata habari kutoka kwa Wamarekani zaidi ya watano. Kwamba siku hii inasherekewa takribani katika shule zote nchini Marekani zikiwepo shule za upili pia. Siku hii haiitwi sikukuu hadi wanaoisherehekea wavute Marijuana kupindukia. Eti kusherehekea mwanzo wa joto ni kisingizio tu; swala kuu ni kusokota Marijuana.

Iwapo utajiuliza maswali ndugu basi hivi ndivyo Marekani inawasaidia wafanyibiashara wa Marijuana. Kumekuwepo fununu pia baadhi ya madaktari Marekani wanawashauri wateja wao kutumia Marijuana. Piga hesabu huku ukitilia maanani mamilioni ya wanafunzi wanaovuta marijuana siku hii 'tukufu'. Siku hii pekee imewazalishia walanguzi wa marijuana mabilioni ya dola.  Baada ya kufanya hesabu, jiulize sheria za U.N. zasemaje kuhusu madawa ya kulevya? Juzi Marekani wamevunja sheria ya U.N. na kushambulia Iraq. Hivi jana wamevunja ya madawa za kulevya kwa kuwaruhusu walanguzi kuuza na wanafunzi kununua.

MAREKANI INAOZA KWA KASI NDUGU. 

April 26, 2006 Posted by | Uncategorized | 4 Comments

UBAKAJI: NJOKI NDUNG’U ANAFICHA HABARI FULANI.

Swala hili lingali halieleweki. Mbunge maalum Njoki Ndung'u amekuwa akijaribu kuwashawishi wabunge wenzake wakubali mswada anaopendekeza; kwamba wabakaji wanastahili kuchukuliwa hatua kali tofauti na jinsi ilivyo sasa. Vikao vingi vimeandaliwa na hivi leo bunge la Kenya ambalo lina wanaume wengi litapitisha au kutopitisha mswada ambao utawafunga wanaume.   

Waitifaki wa mswada huu akiwemo Njoki, wanapokabiliwa na maswali kuhusu mswada wenyewe, habari wanazojitetea nazo ni kama vile ubakaji wa vijisichana vidogo vinapoenda shuleni, ubakaji wa wasichana na wanawake; hivi juzi wamejumulisha habari za kubakwa kwa kinyanya kimoja cha miaka zaidi ya 80. Wanatumia habari hizi kuwafumba wanaume wabunge ili watakapokwenda bunge wapitishe mswada huo mara moja pasi kuupigia maswali.  

Swala fiche ambalo wanawake hawa na baadhi ya wanaume hawataji hata kidogo ni ubakaji wanaosema kwamba umo katika ndoa. Unapochunguza kijelezi cha ubakaji ni kwamba Ubakaji ni kuonyesha dalili au kufanya ngono na mtu pasipo hiari yake au makubaliano; haijalishi mtu yule yumo katika ndoa au la. Ninaposema kuonyesha dalili, ni iwapo utagusa 'vitu' vya mwanamume au mwanamke pasipo hiari yake. Mwanamume akija nyumbani kisha afanye ngono na mkewe pasipo hiari basi huu utaitwa ubakaji. Mwanamume akigusa 'vitu' vya mkewe pasipo hiari yake basi huu utaitwa ubakaji pia.

Hali hii itapelekea wanaume kuwaogopa wanawake maanake ukigusa titi umeingia jela. Aidha wanaume za watu wataishia korokoroni pia kwa sababu waliwakumbatia wake zao au kuwapiga busu pasipo hiari yao. Marekani hivi leo sheria hii inatekelezwa. Madhara yake huku ni kwamba wanaume wamewaogopa wanawake kiasi kwamba mume na mke walioana kwa ndoa takatifu watakuwa na vyumba viwili tofauti vya kulala. Kuna uwezekano kwamba kuzuka kwa ushoga( ndoa za mume-mume au mke-mke) kumesababishwa na wanaume na wanaume kuogopa kuingia jela endapo watagusa 'vitu'.

Ninashuku pia kwamba huyu Njoki Ndung'u anatumiwa kupitisha mawazo ya magharibi barani Afrika. Wametumia nafasi kwamba yeye ni mbunge wa bunge la Afrika na kisha ni mbunge nchini Kenya kupitisha mawazo potovu barani Afrika. Swali ninalojiuliza ni, nani anafadhili vikao vya wabunge kukutania katika hoteli za kifahari ili kupitisha mswada utakaovuruga taasisi ya ndoa.  

Siungi mkono ubakaji wa visichana vidogo au akina nyanya bali ipo haja ya kuongeza katika kijelezi cha ubakaji kwamba ngono katika ndoa halali haitajumulishwa katika kuwatia korokoroni wanaume. Endapo msawada huu utapitishwa pasi kupigiwa maswali kama haya basi wanaume wameangamia. Ni miaka mitano tu na jela nchini Kenya zitajaa wanaume ambao 'wamewabaka' wake zao.

April 26, 2006 Posted by | Uncategorized | 3 Comments

MADHARA YA KUWEPO SARAFU AINA MOJA AFRIKA MASHARIKI.

Vikao vinavyojadili kuungana kwa Afrika Mashariki vimepiga hatua sasa. Aidha kuna bunge sasa na Idara ya sheria ambazo ni mtikati ili mradi huu kuimarika. Marais vilevile wameanza kwa njia fulani kupokezana uenyekiti kwa zamu. Juzi Mheshimiwa Jakaya Kikwete amempokeza Mwai Kibaki Uenyekiti kwa kipindi kinachofuatia.

Aidha ili kuwe muungano imara lazima kuwepo aina moja ya sarafu inayotumika kote Afrika Mashariki. Ina maana kwamba hatutahitaji tena mashilingi ya Kenya, Uganda, Tanzania Rwanda na Burundi iwapo maombi yao ya kujiunga na muungano huu yatapitishwa. Ni kawaida kwamba mataifa yanapoungana wanazua sarafu sawia. Haya yametendeka bara Ulaya. Zaidi ya mataifa 15 yaliyo katika muungano wa European Union yamesahau sarafu zao za awali na kubugia hii iitwayo Euro. Inatarajiwa ni muda mfupi tu na Kronar za Uswidi na Norway hazitakuwapo tena sawa na sarafu za mataifa mengine katika muungano huu.

Nguvu za sarafu inayozaliwa huimarika maradufu tofauti na sarafu za mataifa pweke za awali. Ninachomaanisha ni kwamba iwapo dola 1 ya kimarekani ilibadilishwa kwa  shilingi 70 za Kenya kabla ya kuungana basi huenda dola moja ikanunuliwa kwa shilingi 10 za sarafu itakayozaliwa baada ya kuungana. Iwapo dola moja ilinunuliwa kwa shilingi 1800 za Tanzania basi itanunuliwa kwa shilingi 10 za sarafu mpya.

Athari ya kwanza ya kuwepo na sarafu iliyo na nguvu kupita kiasi ni kwamba raia wa mataifa mbalimbali watalalamika kwamba gharama ya maisha imepanda japo kwa njia tofauti. Watakaoathiriwa zaidi ni raia wa taifa ambalo lilikuwa na sarafu dhaifu kiasi ikilinganishwa na dola. Hivi ndivyo raia wa Uswidi, Norway, na Ujerumani wanalalamika leo. Wanadai gharama ya maisha imepanda kutokana na kuwepo kwa Euro. Hebu angali hali hii, kabla ya muungano wa E.U. sarafu ya Uswidi ilinunuliwa kwa shilingi 9 za Kenya; hivi sasa Euro inanunuliwa kwa shilingi 87 za Kenya.  Hali kama hii itakuwepo mataifa ya Afrika Mashariki yatakapoungana. Dola moja nchini Uganda inanunuliwa kwa zaidi ya shilingi 2000  za Uganda, nchini Tanzania ni zaidi ya shilingi 1500 za Tanzania kisha nchini Kenya ni shilingi 70 za Kenya. Tutakapokuwa na sarafu moja raia wa Uganda watalalamika zaidi ya wenzao kwamba gharama ya maisha imepanda huku raia wa Kenya wakillamika kwa kiasi kidogo tu maanake nguvu za sarafu zaliwa zitapanda kwa kiasi kidogo tu.

Madhara ya pili ni kwamba iwapo haitawekwa sheria ya kulinda uwekezaji, raia wengi wa Kenya wataingia Tanzania na Uganda kwa njia ya kununua ardhi na kuwekeza. Hii ni kwa sababu Wakenya watakuwa na fedha nyingi wakilinganishwa na wenzao Watanzania na Waganda. Sababu ya kuwa na fedha nyingi itatokana na wao kutumia kiasi kidogo cha shilingi za Kenya kununua sarafu mpya. Kwa mfano huenda Wakenya wakabadili sarafu mpya kwa shilingi 5 za Kenya, Watanzania shilingi 20 za Tanzania na Waganda shilingi 50 za Uganda.  Hata hivyo iwapo wasomi Watanzania na Waganda wataruhusiwa kuingia katika soko la Kenya pasipo vikwazo basi hali itakuwa imesawazishwa.

April 21, 2006 Posted by | Uncategorized | 2 Comments

KUNA HATARI YA KALONZO MUSYOKA KUWA RAIS?

            Licha kwamba utafiti wa Steadman umemkweza Kalonzo Musyoka katika ngazi za juu zaidi kuliko wagombea wengine, ipo haja ya Wakenya kumpiga msasa huyu mheshimiwa Kalonzo Musyoka kabla ya kumpa kura zao.  Maswali ambayo tunawza kujiuliza ni , Je alipokuwa waziri wa nchi za kigeni ishughulikia nchi namna gani? Je ana elimu ya kulikwamua taifa kutokana na majanga mengi yanayolikumba? Je mbona mataifa ya magharibi yanampenda zaidi kuliko wagombea wengine? Anahusiana vipi na viongozi wengine?

            Kalonzo ni mwanasheria kutoka chuo kikuu cha Nairobi. Tunaelezwa kwamba ni msemaji bora. Ana ujuzi wa kutetea hoja bungeni na katika vikao vya kimataifa. Kwa kifupi anajua kujieleza vizuri kisheria  kwa lugha ya Kiingereza . Mgombea wa Urais anapokuwa na sifa kama hizi aghalabu mataifa ya magharibi huwa yamepata mwenzao katika kuendeleza unyonyaji wao barani Afrika. Mataifa haya yana hamu kubwa ya rais anayeziheshimu sheria; haijalishi sheria hizo ni za kugandamiza raia au za kuwafaidi. Yatahitaji mtu anayejua katiba na sheria za U.N. anazozielewa vizuri Kalonzo Musyoka. Aidha yanafurahia rais anayejumulisha  kishazi‘ the U.N. declaration….’ katika hotuba zake. Kwa njia hii, huwa wameteka nyara mawazo ya rais na ya raia wanaoongozwa na raiskama yule.  Kwa mfano iwapo Kalonzo ataunga mkono sheria ya U.N. inayosema ‘ mtu ana uhuru wa kuhamia nchi nyingine pasipokuwa vikwazo.’ Mataifa ya magharibi basi watatumia sheria hii kuzoa wataalamu kutoka barani Afrika huku Kalonzo akiendelea kushikilia na kuitetea sheria hii.  

            Pili, kama alivyokuwa Jakaya Kikwete wa Tanzania , Kalonzo alikuwa Waziri wa nchi za kigeni kwa kipindi cha miaka 6. Mgombea wa rais ambaye ana tajriba ya wizara hii huwa ametathminiwa ndani nje na mataifa ya magharibi kupitia hotuba zake za mara kwa mara. Anajulikana vizuri msimamo wake na falsafa yake kulihusu taifa lake. Mataifa haya ya magharibi hunasa hotuba za mawaziri hawa wa nchi za kigeni kisha wanazichunguza na kujua namna ya kumfurahisha anapokuwa rais. Mataifa haya hutafuta namna ya kufyonza zaidi kwa kutumia usemi wa mawaziri hawa. Hivyo basi akina Kikwete na Kalonzo wanapokuwa Marais basi inakuwa heri kwa mataifa haya ya magharibi. Mataifa haya yamezichunguza hotuba za Jakaya Kikwete kwa kipindi cha miaka 10 alipokuwa waziri wa nchi za kigeni na vivyo hivyo wamemjua Kalonzo vizuri alipokuwa waziri wa nchi za kigeni.

            Swala lingine ambalo raia watamshuku Kalonzo ni namna anavyopendeka na mataifa haya ya magharibi. Alipoanzisha Kalonzo ‘Musyoka Foundation’ walikuwepo mabalozi wa Marekani, Ujerumani, miongoni mwa wengine. Ni kawaida mtu anapotaka kitu kutoka kwa mtu fulani kuwa mzuri kupindukia. Hivi ndivyo mtoto huwa anapotaka peremende kutoka kwa mzazi. Inasemekana kwamba licha kwamba Kalonzo hako serikalini kwa sasa, ana athari kubwa sana kwa jinsi ambavyo mataifa ya kigeni yanahusiana na serikali ya Kibaki japo kwa njia fiche. Kwa misingi hii nikidhani kuna malighafi mataifa ya magharibi yamekuwa yakitaka na hili litawezekana tu Kalonzo anapokuwa rais.

            Tofauti na rais Kibaki, Kalonzo hana elimu ya Uchumi ambayo kwa kiasi kikubwa ndio mtikati wa maendeleo ya nchi. Kipindi chote Kibaki amekuwa katika siasa, falsafa yake imekuwa kumaliza umaskini. Hii ndiyo sababu ameamua kuwapa raia nafasi ya kwanza katika ubinafsishaji wa mashirika ya serikali. Sababu iyohiyo imempelekea kuajiri makatibu wa wizara walio na elimu ya uchumi. Vilevile napochunguza baraza lake la Mawaziri lina wataalamu zaidi likilinganishwa na mabaraza ya akina Moi na Kenyatta. Ukitaka kujua falsafa ya Kibaki kwa taifa la Kenya soma Jarida lake ‘Why Kenya needs an economist’. Tofauti nyingine ni kwamba Kibaki ametambua siri ya kunyamaza. Si mzungumzaji wa kiholela kama alivyokuwa Moi na Kenyatta. Anatenda kazi kwa njia ya unyamavu. Polisi walipovamia Standard hakutoa maoni;  vilevile Githongo alipofichua kashfa ya Anglo leasing alinyamaza kimya. Unyamavu ni silaha kubwa ambayo viongozi wa Afrika hawajaitambua. Kunyamaza humfanya mtu kuhesabiwa kuwa mwenye busara. Kunyamaza huwaogofya maadui wa mtu maanake hawajui mwenye kunyamaza anawazia nini. Aghalabu Kibaki amelazimishwa kutoa maoni yake kuhusiana na kashfa mbalimbali lakini ameamua kunyamaza kimya. Alilofanya ni kuwaachisha kazi na kuwafungulia mashtaka wahusika bali hazungumzi katu. Kalonzo kwa upande wake si myamavu japo si mzungumzaji wa kila marakama walivyo Raila na Kenyatta. Taifa la Kenya halihitaji rais 'mdomo wazi' kupita kiasi. Maanake mdomo wazi huwafungulia njia maadui wa nchi yakiwemo mataifa ya magharibi kuzijua siri za serikali na taifa kwa jumla.

April 18, 2006 Posted by | Uncategorized | 105 Comments

NAMNA YA KUPIMA UBORA WA MAISHA.

Kunavyo vigezo mbambali wanavyotumia watu kupima ubora wa maishayao. Baadhi yetu tutatumia mali tuliyonayo kama vile majumba, biashara na mafedha tuliyoweka benki. Wengine tutapima maisha kwa vyeo tulivyo navyo katika jamii kwa mfano mwanasiasa atajiona kuwa bora zaidi kuliko raia wa kawaida. Kisha kunao watatumia elimu kudai kwamba maisha yao ni bora. Hivyo basi profesa atajiona kuwa miongoni mwa watu wachache walio na maisha bora . Wengine watatumia vigezo vya familia. Hivyo basi dume lililo na mke mrembo au watoto watiifu na werevu shuleni atajiona kuwa bora zaidi. Lakini swali linabakia kuwa kilele cha maisha bora ni nini? Ni mapesa, ni vyeo, ni familia, elimu?

         Kwa mujibu wa wanasaikolojia, ubora wa maisha ni jumla ya vipengele vingi. Kipengele kimoja ni jiwe lisiloweza kuijika chungu. Hii ndiyo sababu tajiri aso mke hatakuwa na maisha bora. Hii ndiyo sababu Profesa asokuwa na mali hatajihesabu kuwa na maisha bora. Mwanasiasa asiyekuwa na elimu atajiona duni katika bunge na mara nyingi atanyamaza kimya mijadala inapoendelea bungeni.

         Ukitaka kujua watu uliodhani wana maisha bora sivyo ilivyo, nenda nchini Kenya umpate bwana wa umri wa zaidi ya miaka 50 aliyeamua kujiunga na shule ya msingi licha kwamba anamali. Njoo Marekani ukutane na wanawake wenye dola lakini wameishia katika vyumba vya washauri maanake hawana wenzi katika maisha yao. Rudi nchini Kenya tena ukutane na rais Kibaki ambaye licha ya kudhani kwamba maisha bora ni kuwa rais, ametajwa na upinzani kuwa mhusika katika ufisadi serikalini. Kisha baada ya safari hizo tatu ujilize kwa nini wasomi wengi siku hizi wanajitia kitanzi? Wengi wanajitosa majini, wengine wanajitia mikanda shingoni huku wengine wakibugia sumu.  

            Kwangu mie nikidhani wa ubora maisha hupimwa kwa kiwango cha furaha alicho nacho mtu. Si lazima uwe na mali nyingi kupindukia wala elimu ya hali ya juu ili uwe na furaha. Vilevile furaha hailetwi na cheo alicho nacho mtu katika jamii wala kuwa na familia pekee.

April 15, 2006 Posted by | Uncategorized | 3 Comments

KIFO NI NINI?

Ni peremende tunayoibeba mikobani kila sekunde. Hakibagui tajiri wala maskini. Hakibishi hodi wala hakiambiwi subiri kidogo. Hakitumii aina moja ya usafiri kinapoabiri. Kinawaanua walio kwenye orofa kwa mitetemeko ya ardhi. Kinawazuru maskini kwa kutumia ukame. Kinawatumbuiza mabwanyenye kupitia magonjwa. Kinawamaliza wabunge kwa ajali za ndege. Kinamaliza mataifa makubwa kwa milipuko ya mabomu. Kina nguvu za kuvunja milango ya vyuma tuliyojiwekea. Kinawakamata marais licha yao kuzingirwa na walinzi. Kina mdomo wazi wa kuimeza meli nzima baharini. Umri kwacho si hoja. Kinamtonoa kijana na kumwacha mzee. Hakina huruma eti. Kinafagia familia na kuyaacha mabilioni ya pesa benki.

Kifo ni siri ya MUNGU. Kina vyombo anuwai vya kuabiria. Kikizuru kwangu siku imefika ndugu. Hamna nafasi ya kukiambia njoo mtondogoo.

April 12, 2006 Posted by | Uncategorized | 17 Comments

KITOTO CHA MAREKANI KINASAFIRI ULIMWENGUNI ZAIDI YA MHADHIRI CHUONI AFRIKA.

Kinaya iliyoje? Ukimuuliza mwanafunzi yeyote chuoni Marekani atakwambia ameshazuru Uganda, Uholanzi, Misri, Uswidi na likizo ijayo anaelekea Uhabeshi. Ukimuuliza Mhadhiri wa Sayansi chuoni X katika nchi Y barani Afrika atakwambia kwamba digrii zake zote amezipata nchini Y. Hajawahi hata kusafiri katika mataifa mengine katika bara lake.Ni bayana kwamba nguvu za dola zinawafaidi raia wa mataifa yaliyo na nguvu kiuchumi.

Wahadhiri ni wataalamu ambao wanatakiwa kuwa na uwezo wa kusafiri ulimwengu mzima pasipo kuwekewa vikwazo na ukosefu wa fedha. Hawa ni watu wanaostahili kujua tafiti changa kabisa katika sehemu zingine za ulimwengu.Wakilinganishwa na wahadhiri kutoka Marekani, Wahadhiri wengi barani Afrika ukosefu wa fedha umefungia Wahadhiri katika mazingira ya nchini mwao pekee. Sisemi kwamba hawako radhi kusafiri na kushuhudia tafiti za wengine kote ulimwenguni la hasha, lililopo ni kwamba mishahara wanayopokea haiwaruhusu kushughulikia ya familia kisha waweze kusafiri sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Hii ndio sababu vyuoni barani Afrika tunatumia vitabu vilivyotumika karne zilizopita katika kufundisha wanafunzi. Hii ndio sababu Wahadhiri hawa wanatumia mbinu za ufundishaji zilizopitwa na wakati. Wenzao Marekani wakifunza kupitia tekinolojia ya kisasa wahadhiri barani Afrika wangali wanaandaa vikaratasi usiku kabla ya kuhadhiri siku inayofuata.

Aidha mwanafunzi mfanyikazi wa ziada Chuoni Marekani atapata nauli ya ndege kwa mshahara wa mwezi mmoja akilinganishwa na Professa barani Afrika ambaye licha kwamba ana rundo la digrii anasafiri nchi geni mara moja kila baada ya miaka mitano. Hali hii imepelekea Wahadhiri wetu kuwa na mtazamo finyu wa maeneo yao ya Kitaaluma. Kuna hatari hapa maanake elimu isiyokwenda na wakati inawakwamisha raia badala ya kuwasukuma.

Ili kutatua tatizo hili nikidhani wahadhiri wote duniani wanastahili kuwa na kiwango sawa cha mishahara na marupurupu. Ni kwa kupitia njia hii kwamba watakuwa na uwezo wa kusafiri ili kuhudhuria makongamano na kupata habari mpya kutoka kwa wenzao. Nchi nyingi za kiafrika haziwezi kuwalipa vyema wahadhiri wake. Hivyo basi maoni yangu ni kwamba Umoja wa mataifa (U.N.)unastahili kupewa jukumu la kuwalipa wahadhiri.

April 11, 2006 Posted by | Uncategorized | 2 Comments

KUTOJUMULISHA MIKOPO YA WAFADHILI: HEKO SERIKALI

Utegemezi wa mikopo umeyafanya mataifa mengi kuwa maskini kila kukicha. Sababu ni kwamba wanaoahidi kutoa mikopo huchelea kuitoa au wakakosa kuitoa kabisa. Kisha ikishatolewa wanathibiti namna ya kuitumia na viwango vya riba. Hivi sasa deni la Kenya ni zaidi ya shilingi bilioni 500. Serikali inatumia 15% ya mapato kulipia deni hili.

Hatuwezi kudai kwamba tumefikia kiwango cha maendeleo iwapo tutaendelea kutegemea mikopo kutoka kwa wafadhili. Naipongeza serikali ya Kibaki kwa kutojumulisha mikopo hii katika bajeti inayotazamiwa kusomwa bungeni hivi karibuni. Hii ni ishara njema na zaidi nawapongeza Wakenya kwa kulipa ushuru unapelekea hali hii kuwepo.

April 11, 2006 Posted by | Uncategorized | Leave a comment