kwangila

Just another WordPress.com weblog

MBONA MAREKANI NA UINGEREZA ZINAINGIA TANZANIA BILA BREKI?

Tanzania juzi wamesamehewa madeni. Huzuni iliyoje? Ninaposema huzuni nikidhani Boniphace Makene ananielewa. G8 (mataifa yenye utajiri mkubwa duniani) yalikutana na kuisamehe nchi ya Tanzania madeni. Madeni haya yalikuwa mengi kutoka IMF na World Bank. Si madeni kutoka nchi mahususi kama vile Marekani au Uingereza.

IMF na World Bank ni mali ya mataifa ya ulimwengu. Mataifa mengi yamewekeza katika taasisi hizi mbili. Hivyo basi kusamehewa kwa madeni kuna maana kwamba ni ruzuku kutoka mataifa ya kilimwengu. Hivyo basi hasara kwa washikadau pweke si kubwa mno. Lakini swali Wabongo wanastahili kujiuliza mbona baada ya ruzuku hii Marekani na Uingereza wameingia bila breki kuikopesha Bongo?

Marekani na Uingereza wanajua kwamba wanapochukua nafasi hii kwanza, kabla ya mataifa mengine, basi Tanzania itaanza kulipia mikopo yao kwanza kabla ya kuanza kulipia mikopo mingine kutoka mataifa mengine.

Pili Marekani na Uingereza wametumia fedha nyingi sana katika vita vya Iraq. Hivyo basi wanawekeza mali yao kwa lazima katika mataifa maskini ili izae faida kwa haraka kufidia hasara waliyopata katika vita hivi vya Iraq. Hivyo basi kuna uwezekano mkubwa kwamba faida watakayodai kutokana na mikopo waliyoipa bongo itapanda.

Mataifa haya mawili yamezistadi hotuba za Kikwete na kujua udhaifu wake. Wamejua namna ya kumfurahisha ni kumpa mikopo kwa taifa lake ili kupambana na ufisadi. Kumbuka kuwekeza katika kupambana na ufisadi hakuleti faida ikilinganishwa na iwapo mikopo ile ingewekezwa katika viwanda. Hii ni njia moja ya kuongeza muda wa kulipa mikopo ile. Wanalazimisha mataifa pokezi kutumia mikopo katika miradi isiyoleta faida. Muda unapoongezeka basi ina maana faida kwao kwa kila mkopo.

Nikidhani mataifa haya yanaogopa Marais waliosomea uchumi na siasa maanake wanajua sera zao zitahakikiwa kabla ya misaada yao kukubaliwa. Wabongo mwasemaje?

April 9, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 4 Comments

KAMUSI YA ISIBATI

Kama mwalimu wa Isibati nimeanza kutayarisha kijikamusi cha Isibati kwa Kiswahili. Nawaalika wataalamu wa Isibati kuihakiki kijikamusi hiki kadri ya uwezo wao. Nimelazimika kuswahilisha msamiati mwingi maanake hivi sasa sina suruali, inanibidi niazime kutoka kwa jirani kabla ya kupata suruali yangu. Ongeza visawe, punguza au zua mjadala utakaofanikisha mradi huu. Kamusi yenyewe i hapa chini.

KAMUSI YA ISIBATI 

Kiselelisheni/Accerelation.

Namna ambavyo velositi hubadilika na wakati.

 

Ekwishoni Ajebura (Algebraic Equation)

Ni ekwishoni yenye umbo la f(x)=0: pale ambapo f ni Polinomio

 

Otitudi(Altitude)

Otitudi ya traiango ABC ni mstari kutoka vatekisi moja ya traiango ile hadi kwenye k.m Vatekisi A. Mstari huu hugawa
Mstari BC wa traiango ile kwa vipande sawa.

 

Ango(angle)

Mistari au pleni mbili zinapokutana kinachoundwa ni ango.

 

Wastani wa Kiarithimetiki/Avareji(Arithmetic Mean/Average)

Ni mgao wa hesabu ya vitu na idadi yake. K.m. iwapo thamana ya vitu ni ‘m’ na  idadi ya vitu vile ni ‘n’ basi Avareji yake ni m/n.

 

Besi.(Base)

Katika ekipreshoni xⁿ , X ni besi huku y ikiwa ekisoponenti.

 

Namba bainari.(Binary number)

Ni nambari yenye besi namba 2

 

Baisekiti.(Bisect)

Ni kugawanya mara mbili. Vipande view sawa.

 

Biti.(Bit)

Hii ni dijiti bainari

 

Baiti.(Byte)

Ni kiwango cha memori kinachohitajika kuwakilisha karakita moja katika tarakilishi. Idadi yake huwa ni bit inane.

 

Ango Kati. (Central Angle)

Ni ango iliyo kati ya rediasi mbili.

 

Khodi.(Chord)

Ni mstari unaounganisha pande mbili za kavu Fulani.

 

Duara/ Sako. (Circle)

Umbo mzunguko ambalo sehemu zake huwa na urefu sawa kutoka sehemu iliyo kati.

 

Koni Duara. (Circular cone)

Ni koni ambayo tako

lake
ni duara.

Sakamusenta. (Cicurmcenter)

Sakamusenta ya traiango ni sehemu kati ya duara ilyochorwa ndani ya traiango ile.

 

Koefishienti.(Coefficient)

Ni konsonanti ambayo huzidishwa na kibadiliki Fulani katika polinomio.K.m. katika Polinomio X²+3X+7, Koefishienti ni 1, 3 na 7.

 

Ango Komplimentari. (Complimentary angles)

Hizi ni ango ambazo jumla yazo ni 90°

 

Nambari tata. (Complimentary angles).

Ni jumla ya nambari halisi nay a kufikirika. Km 3+4i pale ambapo i=√-1.

 

Konikevu. (Concave)

Umbo lililopindika ndani.

 

Maumbo kongurenti.(Congruent figures)

Ni maumbo ya kijometriki yanayolingana kwa ukubwa na umbo.

 

Kubu.(Cube).

Ni umbo yambisi lenye mistari sita inayolingana kwa urefu na kufungamana.

 

Ekwishoni kubiki.(Cubic equation)

Ni ekwishoni polinomio ya digrii 3

 

Dekagoni.(Decagon)

Ni polinomio yenye pande 10.

 

Nambari nukta. (Decimal number)

Ni nambari iliyoandikwa kwa kutumia besi 10.

 

Digrii.(Degree)

Digrii ya umbo lolote lile lenye vibadiliki ni ekisiponenti ya variabo/kibadiliki kile. K.m digrii ya 7X³ ni 3.

 

Dinomineta.(Denominator)

Atika nambari mgao x/y, x huitwa numereta nayo y ikatwa dinomineta.

 

Dayagono.(Diagonal)

Katika poligoni mstari unaounganisha vatekisi moja na nyingine isokuwa karibu huitwa dayagono.

 

Dayamita/Diameter

Katika umbo-duara, dayamita ni mstari unaopitia katikati mwa duara ile.

 

Dijiti/Digit

Ni nambari zifuatazo: 0,1,2,3,4,5,6,7,8,9

 

Divaisa/Divisor

Katika nambari mgao a/b, a huitwa dividenti ilihali b ikawa divaisa.

 

Dodekagoni/Dodecagon

Hii ni Poligoni yenye pande 12.

 

Dodekahiduroni/Dodecahedron

Ni umbo yabisi/solid yenye nyuso 12.

 

Domeni/Domain

Domeni ya fankishoni f(x) ni mfululizo wa thamana ambazo x imepewa.

 

Elipsi/Ellipse

Ni umbo pleni ambalo ekwishoni yake ni x²/a²+y²/b²=1

 

Elipusoidi/Ellipsoid.

Ni umbo yambisi ambalo ekwishoni yake ni x²/a²+y²/b²+z²/c²=1

 

Seti tupu/Empty set

Ni seti isokuwa na chochote kile.

 

Poligoni sawa/Equilateral Polygon

Ni poligoni yenye pande zote sawa.

 

Traiangu sawa/Equilateral triangle

Ni traiangu yenye pande zote sawa.

 

Nambari iveni/even number

Ni inteja inayoweza kugawika mara mbili.

 

Ekisiponenti/exponent

Katika ekisipreshoni x², x huitwa besi nayo 2 ikawa ekisiponenti.

 

Fankishoni ekisiponenti

Ni fankishoni f(x)=e²

 

Fakta/factor- Nomino

Ni nambari inayoweza kugawa nyingine sawasawa. Kwa mfano 7 ni fakta ya 28.

 

Fakta/factor- Kitenzi.

Ni kutafuta fakta za nambari Fulani.

 

Fakitorio/factorial

n! (inayotamkwa n fakitorio) ni sawa na kuzidisha nambari zote zilizo kati ya 1 na n. Kwa mfano 3!= 3*2*1 pale ambapo 3 ni n.

 

fomula/formula

Ni namna sifabia ya kuonyesha uhusian kati/baina ya kontiti/quantity mbili au zaidi.

 

Frakishoni/Fraction

Ni ekisipreshoni yenye umbo a/b.

 

Frikwenzi/friquenzi

Ni mara ambazo hali/nambari inatokeza baada ya muda Fulani.

 

Frastamu/Frustum

Katika umbile yambisi k.m. Piramidi au koni isokichwa pleni tako huwa sambamba na pleni juu.

 

 

 

 

 

   

April 9, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 10 Comments

ELIMU YA KISASA INAMDANGANYA MWANAMKE WA KIAFRIKA?

Zama zile hakukuwa elimu hii tunayoipokea. Kungwi, shangazi na nyanya zetu walitwikwa mzigo wa kumuelekeza binti. Elimu kuu ilihusu namna ambavyo anaweza kuishi na mumewe katika ndoa na majukumu yake katika familia japo katika jamii ya waswahili binti alifunzwa pia kumfurahisha mumewe. (Rejelea Utenzi wa Mwanakupona.). Hivyo basi elimu ya msichana ilitofautiana pakubwa na ile ya mvulana.

Ni muhimu nitaje kwamba elimu hii ya kale kwa msichana haikutilia maanani mabadiliko katika gharama za maisha. Jamii zilikuwa na mali nyingi kuanzia mashamba, mifugo n.k. Hivyo basi , mwanamke hakutarajiwa kwenda nje eti kutafuta kazi. Iwapo ni chakula mwanamke aliingia shambani na kuchimbua mhogo. Iwapo ni moto, mwanamke hakwenda dukani kunua gesi, aliingia msituni na kuzoa tita la kuni.

Katika jamii ya kisasa, gharama ya maisha imepanda. Mashamba yamekuwa haba kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu. Vilevile maajilio ya tekinolojia na elimu ya kimagharibi imepelekea msichana kupewa elimu inayoenda na wakati. Lakini swali ni je sababu za kale za kumuelimisha binti zimebadilika au la. Iwapo zimebadilika zina madhara?

Kwa maoni yangu , nikidhani sababu hizi hazifai kubadilika. Elimu ya msichana inafaa kumwandaa kuwa mke bora zaidi kwa mumewe na jamii kwa jumla. Aidha ,anapoelimishwa binti anastahili kuhamasika zaidi kuhusu majukumu yake katika famila. Elimu hii haifai kamwe kumwelekeza msichana kuwa na fikra kwamba hana haja ya mwanamume katika maisha. Binti anapoelimishwa na kuwa Wakili baadaye hastahili kutumia nafasi hii kumea pembe. Huenda mumewe ni maskini wa elimu hivyo basi binti aliye na elimu hafai kamwe kumwona mumewe kama ganda la ndizi. Hastahili kamwe kutumia elimu aliyopata kudharau nafasi ya mumewe katika familia. Kama ilivyo utamaduni wetu waafrika jikoni huwa kwa mwanamke. Mara nyingi wanawake walioelimika wanatumia nafasi hiyo kuwapa zamu waume wao kusonga ugali, kutoa vitoto napkini, n.k. Ikizidi hawa walioelimika watawanyima waume zao haki ya kimsingi pia. Nina maana ya ngono. Baadhi ya wanawake walioelimika wamelishwa mawazo potovu kwamba wana haki ya kukataa kuridhia ngono. Elimu hii vilevile imepelekea wake za watu kuhudhuria vikao/sherehe  pasipo vibali au waume zao kujua wako wapi. Utaajabia kusikia baada ya kazi jioni , mwanamke alihudhuria sherehe ya bosi wake hoteli fulani pasi mumemwe kujua. Hali iliyompelekea kufika nyumbani usiku wa manane.  Labda nitapata makombora hapa kutoka kwa wanawake ambao wanaiona elimu hii inastahili kumpa binti uhuru wa kujifanyia maamuzi mwenyewe.

Ninawavulia kofia wanawake walioelimika na bado wanawapa waume zao heshima wanazostahili. Kuna wanawake Marais, Mawaziri, Maprofesa n.k. ambao huvua vyeo vyao na digrii zao wanapoingia nyumbani. Wakiwa nyumbani hutojua kuwa ni Mahakimu katika mahali pao pa kazi. Hutowasikia wakijibizana na waume zao wanapokatazwa kufanya jambo fulani. Aidha wanawake hawa wamejifunza unyeyekevu katika eilmu waliyoipata na unapowasikiza wanapozungumza utasikia wakiwasifu waume zao. Nilifurahia kusikia daktari mwanamke akimwambia mwanamke mwenzake kwamba ataomba ruhusa kutoka kwa mumewe ya kuhudhuria mkutano.

Iwapo dada mwafrika unadhamiria kutumia elimu kama chambo cha kumgandamiza mumeo umekosea. Wanaume walio wengi wana sifa moja kuu. Sifa yenyewe ni, kasoro za wake zao huwapelekea kutazama nje kuna nani. Haijalishi wake zao wana elimu kiasi gani.Ukimnyima mumeo ngono kwa madai eti una haki ya kukataa maanake umefunzwa hivyo , kesho utamsikia alilala kwa Fatuma. Ukikosa kumpikia chakula utamsikia hotelini na baadaye kwa Subira anayejua kwamba upishi ni jukumu lake.

April 6, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 1 Comment

VIJUSI MBONA TWAAVYA.

Swalingu naulizeni, mnipe jibu makini,

Ngono’zi twazichezani, na mimba twazitoeni,

Kitanda vunja jamani, mapenzi ni buriani,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Kijusi haki kahini, kibali kakupa nani,

Uhai kesha kihini, vituko hivi vya shani,

Bure kakupa manani, uhai nyima kwa nini,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Siambe huna mapeni, mavazi kwako pomoni,

Si’lize mwana talani, minofu wala sokoni,

Siambe ghali sahani, madodo toto mpeni,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Katoa tumbo kinyani, kadungwa sumu sindani,

Katoa tumbo kimbuni, kakata kichwa mwilini,

Katoa tumbo kinyani, katupwa mwana chooni,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Mamangu nakuulizeni, waraka kaandika lini,

Uhondo kawa lahani, kazuka mi kitandani,

Shakawa wazinyonyani, wapandwa kwako shambani,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Katupwa mi’ msituni, majibwa kanitafuna,

Katupwa jana chooni, viwavi nyama kapata,

Metupwa leo mitoni, viboko wote kafuata,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Ya mola kajua nani, kijusi huyu raisi

Ni siri yake maanani, balozi huyu kijusi,

Hakimu yeye Rabani, kijusi huyu ni nesi,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Muzae mwana karani, umupe tasa Halima,

Na mwana hana Mueni, alia wakilalama,

Na mwana usitupeni, peleka mama Fatuma,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Mwenyezi takulaani, rotuba shamba tatowa,

Unapopita njiani, we shoga mate tajawa,

Na kisha ya Firauni, kwa siri ndwele takuwa

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

 

Betizi zakutosheni, ya ziada jalizeni,

Machungwa yamo moyoni, kwa uno uhayawani,

Kijusi kizaliweni, mapanga sikitieni,

Shangazi swali yakini, kijusi mbona twaavya?

April 4, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 2 Comments

HAMNA UBAKAJI KATIKA NDOA.

Mitindo mibaya ya kimagharibi inanyemelea jamii za Kiafrika kwa kasi
mno. Wanawake hasa walioelimika wameambukizwa ndwele na wanaharakati
wanaodai kwamba wanatetea haki za mwanamke. Nikiegemeza mjadala wangu
katika misingi ya dini ya Kikristo ni kwamba haikuwa mapenzi ya MWENYEZI
MUNGU mwanamke kusema kwamba anadai haki zake. Aidha Biblia takatifu
inasema mwanamke anastahili kuwa mnyenyekevu kwa mumewe. Naye mwanamume
ameshauriwa kumpenda mkewe.

Panapo unyenyekevu na mapenzi basi hamna dhana ya ubakaji. Iwapo bwana
ana nyege mkewe anastahili kuwa tayari kumkidhia haja zake. Panapo
mapenzi basi mume atajua kwamba mkewe si panya kiasi cha kujifungua watoto
kila kukicha. Mapenzi vilevile yatapelekea mume kutambua kwamba mkewe
anaugua hivyo basi itakuwa kumuumiza iwapo atadai ngono. 

Dhana hizi za mwanamke aliyeolea kudai kwamba alibakwa na mumewe ni
potovu na zinastahili kupingwa kwa vyovyote vile. Haikosi ndio sababu
wanaharakati hawa wanadai mume na mke ni viumbe sawa. Haiwezekani abadan
katan! Mume aliumbwa kwanza Biblia inasema kisha MUNGU akaona kwamba ipo
haja ya huyu mwanamume kuwa na msaidizi. Hivyo nafasi ya mwanamke
katika jamii inayoongozwa na maadili ya dini ya Kikristo ni ya msaidizi.
Haifai kamwe mwanamke kudai ukurugenzi katika familia.

Ukweli ni kwamba iwapo wanawake wataendelea kubugia sera za magharibi
bila kuzihakiki na kuzipigia maswali basi watajioa wenyewe. Waume zao
watawataliki na walioelimika wataozea nyumbani mwa mama zao.
Watakaobarikiwa ni wale wasio na elimu na wanaotambua uanauke ndio nini. 

April 1, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 12 Comments

MISHAHARA YA WABUNGE INAUMIZA WANANCHI.

Bunge litahudhuriwa na wabunge iwapo mjadala utahusu nyongeza ya mishahara yao. Ijapo mijadala ya jinsi ya kupunguzia raia umaskini basi bunge litahudhuriwa na Kilemi Mwiria peke yake. Hawa 'waheshimiwa' wanajua kuzua mijadala kama vile 'Donde bill', 'Keter bill' n.k. lakini hamna yeyote ameshawahi kuzua mjadala wa 'kupunguza mishahara ya wabunge'.

Ni kosa na laana kubwa kuomba misaada kwa madai eti mnataka kupunguzia raia umaskini kisha badala yake mnajilimbikizia misaada hii kama nyongeza ya mishahara. Nchi inayotegemea misaada kama Kenya haifai kuwa inawalipa wabunge nusu milioni na zaidi. Huyu ni mbunge eti, ijapo waziri basi atapokea milioni mwisho wa mwezi. Haikosi ndio sababu madeni ya Kenya ni mengi kupindukia. Marekani yenyewe isiyokuwa na madeni haiwapi wanasiasa wake kiasi kama hiki cha pesa. Uingereza vilevile tumeelezwa kwamba mmoja wa wanasiasa wake huenda kazini kwa baiskeli.

Ijapo kuomba misaada hata akina Professa Kibwana na wenzake huvua uprofesa na kutia saini misaada hii kuja. Akilini mwao huwazia tu namna ambavyo misaada hii itawasaidia kupokea mamilioni ya pesa kila mwisho wa mwezi. Mradi mlipa kodi ambaye ni raia wa kawaida atalipa, mbona professa ajisumbue kuhakiki athari za mikopo kwa raia wa kawaida? Mirundiko ya madeni kama haya ndiyo yamepelekea ushuru kupanda, na serikali kuanza kuwalazimisha wafanyibiashara kutumia mitambo ya kurekodi mauzo yao.

Nikidhani huu unastahili kuwa mkataba kati ya raia na serikali ijayo mwaka wa 2007. Kwamba tutawapa kura tu iwapo watatuahidi kuwa watapunguza mishahara yao. Hivi ndivyo wakenya wanawaambia akina Uhuru, Kalonzo, Kibaki, Raila, Ruto na Balala. Sijajua sababu ya mwalimu kupokea elfu kumi kisha mbunge kupokea milioni kama mshahara. Je ina maana mbunge hula dhahabu huku mwalimu akila sukuma wiki? Je ina maana kinyesi cha mbunge ni tofauti na cha mwalimu? Je ina maana mbunge huishi mwezini huku mwalimu akiishi duniani?

April 1, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 2 Comments

MIAKA 14: UMRI WA MTOTO KUFANYA KAZI MAREKANI.

Iwapo serikali za bara Afrika zina lengo la kupunguza umaskini, ipo haja ya kuhakiki baadhi ya sheria ambazo hazina mantiki kamwe. Nchini Kenya kwa mfano, raia wamelazimishwa kuamini kwamba ni kinyume cha sheria kumwajiri mtoto akiwa na umri wa chini ya  miaka 18. Kwa king'eng'e wanaiita hali hii 'child labor'.

Kutowatambulisha watoto katika ulimwengu wa kazi kumewafanya kuwa wazembe kiasi cha kununuliwa chupi na mama zao. Nina maana ya watoto walio kati ya umri wa miaka 14-18. Hali hii imepelekea wazazi kutumia rasilimali nyingi kwa watoto kiasi cha kusahau kujali maslahi yao pia. Chukulia kwa mfano mzazi aliye na watoto wanne walio kati ya miaka 14 na 18. Kisha mzazi huyu mshahara wake ni dola 100 kwa mwezi. Mzazi hataweza kuwakidhia watoto hawa mahitaji kwa ubora unaohitajika.Watoto hawa wana umri tosha wa kwenda kusaka kazi hata kama ni ya uyaya au kuosha vyoo. Mradi wapate fedha za kukidhia mahitaji yao.

Nchini Marekani umri wa mtoto kufanya kazi ni miaka 14. Wengi wa watoto walio na umri huu ni wa shule za upili. Baada ya shule jioni, watoto hawa hujitoma katika soko la kazi kutafuta dola. Utawapata wakiosha vyombo katika hoteli, wakifanya uyaya wa muda au kuwatembeza mbwa wa jamaa fulani. Wao hufanya kazi kwa muda kabla ya kwenda nyumbani kufanya mazoezi waliyopewa shuleni. Tajriba hii anayopata mtoto wa Kimarekani humwongezea sifa katika kapu lake siku za usoni atakapotazamia kutafuta kazi ya kudumu.

Nchini Kenya, vitoto vingi hata vyenye umri wa zaidi ya miaka 20 hutarajia wazazi wao kuwakidhia kila takwa. Wanaponing'onozewa kwamba hoteli fulani inahitaji mfanyikazi wa muda vitoto hivi huona hii ni kazi ya wasio na elimu. Itakuwa heri kwao kucheza basketi boli, au kutazama runinga kisha jioni wende nyumbani kuandaliwa chakula.

March 30, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet

UHAKIKI WA WAGOMBEA 4 WA URAIS 2007 NCHINI KENYA.

Walio na hamu ya kuwa rais nchini Kenya wameanza kujinadi sasa. Kila mmoja anajaribu kupiga zumari isikike nje ya eneo lake la uwakishi bunge. Hadi kufikia jana dalili inaonyesha kwamba wanaotaka kupokea mshahara wa zaidi ya milioni mbili kila mwezi wamejikita katika makundi mawili ya kisiasa. ODM na NARC KENYA. Washika dau wakuu katika ODM(Orange Democratic Movement) ni LDP na KANU. Kisha NARC Kenya imeanza kuvutia mabaki ya muungano wa awali(NARC) na baadhi ya vyama vingine kama vile DP. Inadaiwa kwamba Rais Kibaki yuko katika NARC KENYA hata ingawa hajatangaza rasmi. Hata hivyo miongoni mwa wale wanaogombea urais 2007 kunao wanne ambao raia kote nchini wamejinasibisha nao. Hawa ni Mwai Kibaki , Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta.

KIBAKI 

Ana uzamili( Masters) katika maswala ya Kiuchumi kutoka Makerere. Amekuwa makamu wa rais miaka ya 80 kabla ya kuwa waziri wa fedha miaka ya 70. Amekuwa kiongozi rasmi wa upinzani baada ya kujiuzulu kutoka KANU. Ana umri wa zaidi ya miaka 70. Anatokea katika jamii ya Wakikuyu ambao ndio wengi nchini Kenya. Hivi sasa ni rais wa Kenya. Amekuwa mbunge Nairobi kabla ya kuhamia nyumbani. Ana zaidi ya miaka 30 katika siasa. Ni mkatoliki. Haijulikani iwapo yuko NARC au ni NARC KENYA.

KALONZO MUSYOKA

Ana shahada katika sheria kutoka Nairobi. Amekuwa waziri wa nchi za kigeni katika serikali ya KANU. Amekuwa waziri katika wizara zaidi ya nne katika maisha yake ya uanasiasa. Wiizara zenyewe ni Utalii, Elimu, Mazingira  Utalii n.k.  Ana umri wa kati ya 52 na 55. Amekuwa mwanasiasa mwaminifu katika enzi ya KANU. Hajahusishwa na kashfa zozote zile za ufisadi. Amekuwa mhakiki katika serikali ya Kibaki hali iliyopelekea yeye kuachishwa kazi kama waziri. Ana zaidi ya miaka 20 katika siasa. Amekuwa mstari wa mbele kufanikisha amani Sudan na Somalia. Hivi sasa yuko katika LDP, tawi la ODM. Anatokea katika jamii ya Wakamba mkoa wa Mashariki.

RAILA ODINGA.

Ana uzamili katika Uhandisi kutoka Ujerumani. Amekuwa katika upinzani tangia alipoingia katika siasa. Hata hivyo amekuwa serikali ya KANU kwa muda mfupi  na vile vile katika serikali ya Kibaki. Ana uwezo wa kuvuta umati kwa namna anavyotumia lugha. Ni mbunge Nairobi licha kwamba anaathiri pakubwa siasa mkoani Nyanza anakotokea. Ametiwa korokoroni kwa msimamo wake sugu wa kisiasa katika miaka ya 80. Ana umri wa miaka 60. Amekuwa waziri wa ujenzi wa barabara kabla ya kutimuliwa kutoka katika serikali ya Kibaki. Kiwanda wanachomiliki kama familia kimetajwa katika uchunguzi wa ufisadi nchini. Yuko katika LDP tawi la ODM

UHURU KENYATTA.

Amelelewa kwa utashi tangu alipotungwa tumboni mwa mamaye. Babake alikuwa mwanzilishi wa taifa. Ana digrii ya siasa na uchumi kutoka Marekani. Amekuwa Marekani kwa muda mrefu kabla ya kuja nyumbani kupokea uongozi wa KANU kutoka kwa Daniel Moi. Ana umri wa kati ya miaka 43 na 48. Ana biashara kibao. Amegombe ubunge wakati fulani na kuukosa hadi alipopendekezwa kugombea urais. Anatokea katika jamii ya wakikuyu mkoa wa kati. Hivi sasa ni kiongozi rasmi wa upinzani. Aliongoza msafara hadi Uingereza kumuhoji aliyekuwa katibu wa maadili kuhusu kashfa ya Anglo Leasing( ufisadi katika serikali ya kibaki). Yuko katika KANU tawi la ODM

March 30, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet

GHARAMA YA KUCHAGUA RAIS MPYA KILA BAADA YA MIAKA 5.

Hata ingawa wananchi nchini Kenya watachangamkia kuchagua rais mpya kila baada ya miaka 5, kuna gharama fiche ambayo raia hawajaitambua. Nchini Kenya tumewastaafisha marais wawili sasa; Jommo Kenyatta na Daniel Moi.

Rais anapostaafu ina maana kwamba anastahili kupokea marupurupu ya uzeeni. Nikirejelea mfano wa Mstaafu Daniel Moi, marupurupu aliyopokea ni mengi sana. Tukianza na maelfu ya pesa anazopokea kila mwezi, kisha ulinzi na magari yanayotiwa mafuta, kuendeshwa na kurekebishwa kwa ushuru unaotozwa wananchi. Hali ni vivyo hivyo nyumbani kwa Jommo Kenyatta.

Tuchukulie kwa mfano, Kibaki atashindwa katika uchaguzi ujao, atakuwa ametumikia nchi kwa miaka 5. Tuchukulie pia atakayetwaa mamlaka atashindwa katika uchaguzi wa 2012. Iwapo hali itakuwa hivyo kwa kipindi cha miaka 20 ina maana kwamba tutakuwa na marais 6 wanaopokea marupurupu kutoka katika ushuru unaotozwa raia.

Marupurupu wanayopewa marais wastaafu nchini Kenya ni mengi. Na mtindo kama huu ni wa kufilisisha umma badala ya kuwahudumia. Maoni yangu ni kwamba rais anastahili kupewa nafasi ya miaka 10 kuongoza nchi. Iwapo wananchi wameridhishwa na uongozi wake basi anaweza kugombea urais zaidi na zaidi.  

Hata ingawa uongozi wa Moi kwa miaka 24 uliandamana na ufisadi, kwa kiasi fulani haukupelekea kunyonywa kwa mfuko wa umma kwa misingi eti marupurupu ya rais anayestaafu. Tungebadili rais kila baada ya miaka 5 katika kipindi hiki Moi alikuwa mamlakani ina maana kwamba hivi sasa tungekuwa na marais 6 wanaopokea marupurupu kutoka kwa mfuko wa umma.

Nikidhani hii ndiyo sababu ya baadhi ya mataifa kudumisha uongozi wa kifalme. Hii ni kwa sababu kuna familia moja tu iliyo mamlakani, hivyo basi matumizi ya fedha za umma yanakuwa machache kuliko mataifa yanayobadili rais kila baada ya muda fulani.

Kwa misingi hii ya kiuchumi basi Kibaki anastahili kupewa miaka mingine 5 uongozini. Kazi yake ikiwa nzuri mwishoni na awe na hamu ya kugombea tena basi wananchi wanastahili kumpa kura.   

March 29, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 1 Comment

KENGEN YAUZA HISA SASA.

Ndugu zangu Wakenya wana habari kwamba KENGEN( Shirika pweke la usambazaji umeme Kenya) inauza 30% ya hisa zake kwa umma. Kwa Wakenya ni shilingi 11.90 za Kenya kisha kuna bei ya raia kutoka TZ na Uganda ambayo ni nafuu kiasi kuliko ya wageni kutoka nchi zingine.

KENGEN ni mojawepo ya mashirika ambayo hadi sasa yanamilikiwa na serikali. Historia inaonyesha kwamba KENGEN imekuwa ikipata faida tangu ilipoanzishwa. Hii ni mara ya kwanza tangu Kenya kupata uhuru Serikali kujaribu kuwapunguzia raia umaskini kwa kuweka mazingira mufti ya uwekezaji.

Hisa zimeanza kuuzwa tarehe 20 machi na itafungwa tarehe 14 Aprili. Panapo majaliwa huenda mwisho wa mwaka thamana ya hisa hizi itakuwa imepanda hadi kufikia zaidi ya shilingi 50 za Kenya. Hivyo itakuwa faida kwa yeyote ambaye atakuwa amewekeza.

Kwa WaTZ mnaweza kuwatuma jamaa zenu Kenya katika Kenya Commercial Banks ili waweze kuwanunulia hisa kabla ya kipindi kufungwa. Iwapo mtahitaji habari na usaidizi zaidi niko tayari kuwapa maanake tunaelekea kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

March 28, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 2 Comments