kwangila

Just another WordPress.com weblog

MAREKANI INAVYOFADHILI VITA BARANI AFRIKA.

Habari kwamba Marekani inawafadhili mibabe wa vita nchini Somalia inastahili kuwaamsha viongozi wa bara la Afrika na ulimwengu kwa jumla. Tangu 1992 hakujakuweko serikali nchini Somalia baada ya nchi hiyo kusombwa na mizozo ya kikabila. Serikali ya Siyad Barre ililazimika kung'atuka baada ya baadhi ya mibabe wa kivita kuziongoza jamii zao dhidi ya serikali. Hali hii ilipelekea Wasomali wengi kukikimbilia nchini Kenya. Hivi sasa kuna zaidi ya Wakimbizi 100,000 katika kambi ya Wakimbizi ya Daadab Kaskazini Mashariki mwa Kenya. Ni muhimu kutaja kwamba katika zile harakati za vita vya  kikabila, Wasomali wengi waliuawa, wengine kubakwa , wengine walitafunwa na wanyama pori na zaidi wengine wamekuwa walemavu wa kudumu.

Katika mwaka wa 2004 serikali ya mpito iliundwa rais wake akiwa Rais Abdullahi Yusuf. Haya yote yalifanyikia Nairobi maanake pilipili ilikuwa imetapakaa kote mjini Mogadishu na miji mingine. Hata hivyo ilibidi Serikali ya Adullahi kuhamishwa hadi mji salama kiasi wa Johar nchini Somalia baada ya shinikizo kutoka jamii ya kimataifa. Serikali hii haingeweza kupata makazi Mogadishu maanake mibabe wa vita wenye silaha kali wangali wanathibiti kila kitu jijini Mogadishu. Asilimia kubwa ya serikali hii ya Abdullahi ni mibabe wa kivita ambao ni sugu hata hivi leo. Hawakubaliani kwa asilimia 100 na sera zinazopitishwa na bunge.

Licha kwamba serikali ipo sasa, Abdullahi amedai kwamba Marekani inawafadhili mibabe wa kivita badala ya kuifadhili serikali kupitia taasisi zinazostahili kutumika. Alisema haya nchini Uswidi na zaidi akasema kwamba Marekani haiko radhi kuona kwamba nchi hii ya Somalia ina amani. Aidha ufadhili wanaopata mibabe hawa unawapelekea kuwa sugu zaidi kiasi kwamba hawasikii lolote analosema Abdullahi. Hawatambui katu kwamba kuna rais, kazi yao ni kushirikiana na Marekani kuongeza vita nchini Somalia kwa madai eti wanayawinda makundi ya Ki-Alqaida. Bwana wao sasa ni Marekani bali sio Abdullahi.

Mataifa mengine barani Afrika ambayo yamesombwa katika mizozo barani Afrika ni yale yenye mafuta na madini adimu duniani. Mifano ya mataifa haya ni Sudan, Nigeria, Congo, n.k. Nitarejelea Sudan pekee katika mjadala huu. Je Marekani inachangia vipi katika mzozo wa Darfur nchini Sudan?

Eneo la Darfur linajulikana kama lenye mafuta na kwa muda mrefu limekuwa kitega uchumi cha serikali ya Sudan. Marekani haifurahishwi na uamuzi wa serikali ya Sudan kuuzia mafuta mataifa mengine mbali sio Marekani. Marekani ilipotaambua hili, iliamua kumtumia John Garang kuipiga vita serikali. Marekani iliwahami wanajeshi wapinzani wa SPLA na SPLM walioongozwa na John Garang. Swala kuu lilikuwa  Sudan kusini iwe taifa huru. Kwa njia hii Marekani ingeweza kushauriana na serikali ya John Garang (ambaye angekuwa rais wa Sudan Kusini )bila kuomba ruhusa kutoka kwa el-Bashir. Hta hivyo Garang aliaga katika ajali ya ndege pindi tu mkataba ulipotiwa saini jijini Nairobi. Hali hii ilipelekea makamu wake Savar Kiir ambaye hana elimu yoyote kuchukua hatamu za uongozi. Kubuka John Garang alikuwa Daktari kando ya kuwa mwanajeshi.

Katika mifano hii miwili ya Somalia na Sudan, ni wazi kwamba kuwepo mizozo barani Afrika kunafadi Marekani. Wanafaidika na wakimbizi maanake wanawahamisha baadaye hadi nchini Marekani kufanya kazi za kishenzi. Habari nilizopokea hivi juzi ni kwamba Marekani inawahamisha wakimbizi zaidi ya 30,000 kuja Marekani kufanya kazi. Nilidhibitisha haya nilipowazuru Wakimbizi wa Kisomalia ambao wanaishi Providence nchini Marekani. Aliyesema utumwa ulitoweka ungalipo hadi hivi leo hasa katika uhusiano wa Marekani na Mataifa yenye mizozo barani Afrika.

Faida ya pili wanayolenga Wamarekani ni kutokana na kuwepo mizozo ni mafuta kwa ajili ya magari yake, ndege na kupasha vyumba joto wakati wa baridi. Unaposikia Marekani inatafuta mafuta barani Afrika imebeba silaha kwa mkono wa kushoto ili kuwapa wapinzani wa serikali endapo itanyimwa mafuta. Si eti Marekani haina mafuta yake, bali wanahifadhi rasilimali zao kwanza, watumie visima vya ulimwengu kisha  warudie kuchimba vyao visima vya ulimwengu vinapokauka. Hii ndiyo sababu ninashuku kushuka mizozo katika mataifa yanayoipa Marekani leseni ya kuchimba visima nchini mwao. Ni wazi kwamba baada ya mataifa ya mashariki ya kati kutambua ushetani wa Marekani, yameanza kukatiza kiasi cha mafuta yanayokwenda Marekani. Halli hii inapelekea Marekani kuanza kuchimba mafuta barani Afrika. Hii ni dalili ya mizozo zaidi barani Afrika siku za usoni. 

May 9, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 7 Comments

MISHAHARA YA WABUNGE KENYA: WIZI! WIZI! WIZI!

 

Uingereza  ni mojawepo ya nchi zenye utajiri mkubwa duniani. Katika mwaka wa 2005, nchi hii ilikuwa na GDP pakapita ya $30,900. Yaani ukigawa pato la nchi kwa idadi yote ya wananchi mwakani 2005.  Katika vipimo hivi
Kenya ni mojawepo ya nchi maskini zaidi ulimwenguni. Katika mwaka wa 2005 GDP pakapita ya Kenya ilkuwa $1,200.

Uingereza inamlipa Waziri wake mkuu Ksh milioni 22 kila mwaka.
Kenya inamlipa Mkurungenzi wa Ufisadi nchini Ksh Milioni 30 kila mwaka. Rais Kibaki naye anapata Ksh milioni 24 kila mwaka. Aidha rais Kibaki anapata mshahara mkubwa zaidi ya Waziri mkuu wa Uingereza kwa shilingi Ksh milioni 2 kila mwaka.

Mawaziri nchini Kenya, manibu wao, wabunge ni mojawepo ya watu wanaopokea mishahara ya juu zaidi ulimwenguni kote. Haya yanaendelea wakati ambapo tunawapigia magoti Ungereza na wafadhili wengine kutupa mikopo. Zaidi ya hayo raia wanakufa kwa ajili ya ukame na janga la ukimwi.

Watu hasa wanaostahili nyongeza hii ni walimu, madaktari, waugzi, wafanyikazi wa serikali, ambao hupata mapeni tu baada ya kulala barabarani wakidai nyongeza ya mishahara. Aidha hawa wabunge walafi kama fisi wana huduma nyinginezo nyingi ambazo wanazipokea. Wana pensheni bora zaidi ulimwenguni, huduma za matibabu, bima na marupurupu ya kujinunulia magari ya kifahari.  Isitoshe ni nadra sana kwa hawa kulipa ushuru. Abdulahi ambaye mifugo wake wafa njaa na Musyoki ambaye wanawe wafa njaa ndio wanatozwa ushuru unaowalipa hawa fisi.

Ukitaka kujua ushetani wa mambo haya, tazama tabia zao mjadala unaporushwa hewani kuhusu nyongeza yao ya mishahara.  Raila atakuwa rafikye Kibaki, Ruto ataongea vizuri na Karua. Swala la pesa linawaleta pamoja na wanaliunga mkono pasi Tuju au Balala kukenua kinywa.  Mishahara inapotajwa hamna, ODM , NARC, au CHAMA cha MAPINDUZI.  Wote wanakuwa mapaka wakati huu waking’ang’ania paketi ya maziwa.

Nchini Marekani vuguvugu la kisiasa kwa jina Boston Tea Party, lilipelekea wafanyibiashara, na raia kuandamana kwa ajili ya kile walichokiita ‘utozwaji ushuru kulipa huduma zisizokuwepo’. Kwa mkabala huo, Uingereza ilipokuwa mkoloni wa ulimwengu iliwatoza wakoloniwa ushuru pasi kuwashirikisha abadan kataan katika kutoa maamuzi. 

  Aidha raia hawangekuwa na chuki endapo nyongeza ya mishahara inandamana na utendaji kazi.  Linalonisikitisha ni kwamba utendaji wa wengi wa wabunge hawa ni butu. Kazi yao ni kupinga miradi ya kufaidi raia ili waweze kuwa na silaha ya kushambulia serikali na kurudi bunge baada ya miaka mitano. Kwa sababu wameonyesha kwamba nia yao ni kuvuna kadri ya uwezo wao ni dhahiri kwamba hawa wenye matumbo makubwa hawako tayari kuhudumia raia. Hawafai kamwe kuwa ndio wanajiwekea kiwango cha mshahara na kutuwekea kiwango cha ushuru tunachostahili kulipa.

Iwapo hakimu Aaron Ringeera angekuwa amewatia baadhi ya hawa jela angalau tungesema anastahili kulipwa nusu ya mshahara wake bali sio milioni 30 kwa mwaka. Lakini bwana huyu mtoka Meru ameishia kuwatia korokoroni wauzaji sukumawiki na waoshaji vyoo eti kwa sababu hawajalipa ushuru na kamwe hatawagusa wabunge na mawaziri. Si eti hamna ushahidi wa kuwatia vizuizini wabunge. Ripoti za Mhasibu mkuu na kamati za bunge zimetoa mapendekezo ya baadhi ya wabunge hawa kuhukumiwa ‘kifo’ kwa ufisadi wanaouendeleza. Kwa misingi hii basi Ringeera anakuwa fahali asoweza kutungisha mamba; Simba kibogoyo anayewinda nzi badala ya nyati.

Nina uhakika hamna mbunge hata mmoja anayewatetea maskini. Wanaojaribu wanacheza siasa ili waonekane wanajinasibisha na maskini lakini wapi. Kalonzo juzi amesema nyongeza ya mishahara haifai sasa. Je umemsikia akisema kwamba nyongeza aliyopewa ataitoa kwa akina Wambua wenye njaa huko Mwingi Kaskazini? 

Wapigaji kura tunastahili kukataa tabia hii maradufu kabla ya nchi kutangazwa haina pesa zozote. Tuamke zaidi ya vile tuliamka tulipokataa katiba tupiganie usambazaji sawa wa utajiri wan nchi. Ukweli ni kwamba hamna mbunge(awe katika serikali au upinzani) atakayetuunga mkono katika vita hivi maanake tunajaribu kupunguza kiasi cha ugali katika sahani zao. Tutafanikiwa kwa kuokota sahihi za raia wanaopinga nyongeza ya mishahara. Tukishapata mamilioni ya sahihi tuwapelekee wabunge pia watie sahihi. Atakayekataa, tumwondoe katika orodha ya wagombea 2007. Baada ya hapo tutumie kipengele hiki kuwageza wagombea wa Urais. Akina Raila, Kibaki , Kalonzo, Balala na wengine wanastahili kuchaguliwa endapo watakubali kupunguza mishaharayao na ya wabunge wenzao. Anayekataa aondolewe katika orodha ya wagombe wa Urais.

Tukishapata M/Wagombea wa Urais, tulazimishe kuunda kwa kamati isokuwa na mbunge yeyote itakayotathmini mishahara ya wabunge.Baada ya kamati kuundwa tulazimu, wabunge kulipa ushuru pia. Sote Wakenya twenda msalani. Hakuna wakudai kwamba kinyesi chake ni cha dhahabu. Hivyo kila mmoja anastahili kulipa ushuru. Huu ndio utakuwa mkataba wetu na serikali ijayo.     

 

May 2, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 6 Comments