KUNA HATARI YA KALONZO MUSYOKA KUWA RAIS?
Licha kwamba utafiti wa Steadman umemkweza Kalonzo Musyoka katika ngazi za juu zaidi kuliko wagombea wengine, ipo haja ya Wakenya kumpiga msasa huyu mheshimiwa Kalonzo Musyoka kabla ya kumpa kura zao. Maswali ambayo tunawza kujiuliza ni , Je alipokuwa waziri wa nchi za kigeni ishughulikia nchi namna gani? Je ana elimu ya kulikwamua taifa kutokana na majanga mengi yanayolikumba? Je mbona mataifa ya magharibi yanampenda zaidi kuliko wagombea wengine? Anahusiana vipi na viongozi wengine?
Kalonzo ni mwanasheria kutoka chuo kikuu cha Nairobi. Tunaelezwa kwamba ni msemaji bora. Ana ujuzi wa kutetea hoja bungeni na katika vikao vya kimataifa. Kwa kifupi anajua kujieleza vizuri kisheria kwa lugha ya Kiingereza . Mgombea wa Urais anapokuwa na sifa kama hizi aghalabu mataifa ya magharibi huwa yamepata mwenzao katika kuendeleza unyonyaji wao barani Afrika. Mataifa haya yana hamu kubwa ya rais anayeziheshimu sheria; haijalishi sheria hizo ni za kugandamiza raia au za kuwafaidi. Yatahitaji mtu anayejua katiba na sheria za U.N. anazozielewa vizuri Kalonzo Musyoka. Aidha yanafurahia rais anayejumulisha kishazi‘ the U.N. declaration….’ katika hotuba zake. Kwa njia hii, huwa wameteka nyara mawazo ya rais na ya raia wanaoongozwa na raiskama yule. Kwa mfano iwapo Kalonzo ataunga mkono sheria ya U.N. inayosema ‘ mtu ana uhuru wa kuhamia nchi nyingine pasipokuwa vikwazo.’ Mataifa ya magharibi basi watatumia sheria hii kuzoa wataalamu kutoka barani Afrika huku Kalonzo akiendelea kushikilia na kuitetea sheria hii.
Pili, kama alivyokuwa Jakaya Kikwete wa Tanzania , Kalonzo alikuwa Waziri wa nchi za kigeni kwa kipindi cha miaka 6. Mgombea wa rais ambaye ana tajriba ya wizara hii huwa ametathminiwa ndani nje na mataifa ya magharibi kupitia hotuba zake za mara kwa mara. Anajulikana vizuri msimamo wake na falsafa yake kulihusu taifa lake. Mataifa haya ya magharibi hunasa hotuba za mawaziri hawa wa nchi za kigeni kisha wanazichunguza na kujua namna ya kumfurahisha anapokuwa rais. Mataifa haya hutafuta namna ya kufyonza zaidi kwa kutumia usemi wa mawaziri hawa. Hivyo basi akina Kikwete na Kalonzo wanapokuwa Marais basi inakuwa heri kwa mataifa haya ya magharibi. Mataifa haya yamezichunguza hotuba za Jakaya Kikwete kwa kipindi cha miaka 10 alipokuwa waziri wa nchi za kigeni na vivyo hivyo wamemjua Kalonzo vizuri alipokuwa waziri wa nchi za kigeni.
Swala lingine ambalo raia watamshuku Kalonzo ni namna anavyopendeka na mataifa haya ya magharibi. Alipoanzisha Kalonzo ‘Musyoka Foundation’ walikuwepo mabalozi wa Marekani, Ujerumani, miongoni mwa wengine. Ni kawaida mtu anapotaka kitu kutoka kwa mtu fulani kuwa mzuri kupindukia. Hivi ndivyo mtoto huwa anapotaka peremende kutoka kwa mzazi. Inasemekana kwamba licha kwamba Kalonzo hako serikalini kwa sasa, ana athari kubwa sana kwa jinsi ambavyo mataifa ya kigeni yanahusiana na serikali ya Kibaki japo kwa njia fiche. Kwa misingi hii nikidhani kuna malighafi mataifa ya magharibi yamekuwa yakitaka na hili litawezekana tu Kalonzo anapokuwa rais.
Tofauti na rais Kibaki, Kalonzo hana elimu ya Uchumi ambayo kwa kiasi kikubwa ndio mtikati wa maendeleo ya nchi. Kipindi chote Kibaki amekuwa katika siasa, falsafa yake imekuwa kumaliza umaskini. Hii ndiyo sababu ameamua kuwapa raia nafasi ya kwanza katika ubinafsishaji wa mashirika ya serikali. Sababu iyohiyo imempelekea kuajiri makatibu wa wizara walio na elimu ya uchumi. Vilevile napochunguza baraza lake la Mawaziri lina wataalamu zaidi likilinganishwa na mabaraza ya akina Moi na Kenyatta. Ukitaka kujua falsafa ya Kibaki kwa taifa la Kenya soma Jarida lake ‘Why Kenya needs an economist’. Tofauti nyingine ni kwamba Kibaki ametambua siri ya kunyamaza. Si mzungumzaji wa kiholela kama alivyokuwa Moi na Kenyatta. Anatenda kazi kwa njia ya unyamavu. Polisi walipovamia Standard hakutoa maoni; vilevile Githongo alipofichua kashfa ya Anglo leasing alinyamaza kimya. Unyamavu ni silaha kubwa ambayo viongozi wa Afrika hawajaitambua. Kunyamaza humfanya mtu kuhesabiwa kuwa mwenye busara. Kunyamaza huwaogofya maadui wa mtu maanake hawajui mwenye kunyamaza anawazia nini. Aghalabu Kibaki amelazimishwa kutoa maoni yake kuhusiana na kashfa mbalimbali lakini ameamua kunyamaza kimya. Alilofanya ni kuwaachisha kazi na kuwafungulia mashtaka wahusika bali hazungumzi katu. Kalonzo kwa upande wake si myamavu japo si mzungumzaji wa kila marakama walivyo Raila na Kenyatta. Taifa la Kenya halihitaji rais 'mdomo wazi' kupita kiasi. Maanake mdomo wazi huwafungulia njia maadui wa nchi yakiwemo mataifa ya magharibi kuzijua siri za serikali na taifa kwa jumla.
-
Recent
- MAREKANI INAVYOFADHILI VITA BARANI AFRIKA.
- MISHAHARA YA WABUNGE KENYA: WIZI! WIZI! WIZI!
- SIKUKUU YA KUVUTA MARIJUANA MAREKANI.
- UBAKAJI: NJOKI NDUNG’U ANAFICHA HABARI FULANI.
- MADHARA YA KUWEPO SARAFU AINA MOJA AFRIKA MASHARIKI.
- KUNA HATARI YA KALONZO MUSYOKA KUWA RAIS?
- NAMNA YA KUPIMA UBORA WA MAISHA.
- KIFO NI NINI?
- KITOTO CHA MAREKANI KINASAFIRI ULIMWENGUNI ZAIDI YA MHADHIRI CHUONI AFRIKA.
- KUTOJUMULISHA MIKOPO YA WAFADHILI: HEKO SERIKALI
- MBONA MAREKANI NA UINGEREZA ZINAINGIA TANZANIA BILA BREKI?
- KAMUSI YA ISIBATI
-
Links
-
Archives
- May 2006 (2)
- April 2006 (14)
- March 2006 (12)
-
Categories
-
RSS
Entries RSS
Comments RSS