kwangila

Just another WordPress.com weblog

KITOTO CHA MAREKANI KINASAFIRI ULIMWENGUNI ZAIDI YA MHADHIRI CHUONI AFRIKA.

Kinaya iliyoje? Ukimuuliza mwanafunzi yeyote chuoni Marekani atakwambia ameshazuru Uganda, Uholanzi, Misri, Uswidi na likizo ijayo anaelekea Uhabeshi. Ukimuuliza Mhadhiri wa Sayansi chuoni X katika nchi Y barani Afrika atakwambia kwamba digrii zake zote amezipata nchini Y. Hajawahi hata kusafiri katika mataifa mengine katika bara lake.Ni bayana kwamba nguvu za dola zinawafaidi raia wa mataifa yaliyo na nguvu kiuchumi.

Wahadhiri ni wataalamu ambao wanatakiwa kuwa na uwezo wa kusafiri ulimwengu mzima pasipo kuwekewa vikwazo na ukosefu wa fedha. Hawa ni watu wanaostahili kujua tafiti changa kabisa katika sehemu zingine za ulimwengu.Wakilinganishwa na wahadhiri kutoka Marekani, Wahadhiri wengi barani Afrika ukosefu wa fedha umefungia Wahadhiri katika mazingira ya nchini mwao pekee. Sisemi kwamba hawako radhi kusafiri na kushuhudia tafiti za wengine kote ulimwenguni la hasha, lililopo ni kwamba mishahara wanayopokea haiwaruhusu kushughulikia ya familia kisha waweze kusafiri sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Hii ndio sababu vyuoni barani Afrika tunatumia vitabu vilivyotumika karne zilizopita katika kufundisha wanafunzi. Hii ndio sababu Wahadhiri hawa wanatumia mbinu za ufundishaji zilizopitwa na wakati. Wenzao Marekani wakifunza kupitia tekinolojia ya kisasa wahadhiri barani Afrika wangali wanaandaa vikaratasi usiku kabla ya kuhadhiri siku inayofuata.

Aidha mwanafunzi mfanyikazi wa ziada Chuoni Marekani atapata nauli ya ndege kwa mshahara wa mwezi mmoja akilinganishwa na Professa barani Afrika ambaye licha kwamba ana rundo la digrii anasafiri nchi geni mara moja kila baada ya miaka mitano. Hali hii imepelekea Wahadhiri wetu kuwa na mtazamo finyu wa maeneo yao ya Kitaaluma. Kuna hatari hapa maanake elimu isiyokwenda na wakati inawakwamisha raia badala ya kuwasukuma.

Ili kutatua tatizo hili nikidhani wahadhiri wote duniani wanastahili kuwa na kiwango sawa cha mishahara na marupurupu. Ni kwa kupitia njia hii kwamba watakuwa na uwezo wa kusafiri ili kuhudhuria makongamano na kupata habari mpya kutoka kwa wenzao. Nchi nyingi za kiafrika haziwezi kuwalipa vyema wahadhiri wake. Hivyo basi maoni yangu ni kwamba Umoja wa mataifa (U.N.)unastahili kupewa jukumu la kuwalipa wahadhiri.

April 11, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 1 Comment

KUTOJUMULISHA MIKOPO YA WAFADHILI: HEKO SERIKALI

Utegemezi wa mikopo umeyafanya mataifa mengi kuwa maskini kila kukicha. Sababu ni kwamba wanaoahidi kutoa mikopo huchelea kuitoa au wakakosa kuitoa kabisa. Kisha ikishatolewa wanathibiti namna ya kuitumia na viwango vya riba. Hivi sasa deni la Kenya ni zaidi ya shilingi bilioni 500. Serikali inatumia 15% ya mapato kulipia deni hili.

Hatuwezi kudai kwamba tumefikia kiwango cha maendeleo iwapo tutaendelea kutegemea mikopo kutoka kwa wafadhili. Naipongeza serikali ya Kibaki kwa kutojumulisha mikopo hii katika bajeti inayotazamiwa kusomwa bungeni hivi karibuni. Hii ni ishara njema na zaidi nawapongeza Wakenya kwa kulipa ushuru unapelekea hali hii kuwepo.

April 11, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet