kwangila

Just another WordPress.com weblog

WIZARA YA NCHI ZA KIGENI AFRIKA MASHARIKI.

Nchi zilizoendelea zimejua kutambua vipawa vya wanasiasa wakiwa wangali vijana. Katika hali hii kipawa cha mwanasiasa kinapotambulika, yeye huwekwa katika mazingira ambamo yatamsaidia kukuza kipawa kile ili labda siku za usoni aweze kufaidi nchi akiwa na tajriba toshelevu. Nchini Marekani kwa mfano, chama cha upinzani kimetambua kipawa cha Barrack Obama; na inasemekana kwamba licha ya yeye kuwa Mmarekani mweusi, ana nafasi nzuri hata ya kuwania Urais siku za usoni. Hivyo basi ,amekuwa malighafi ya kutegemewa katika kuzua na kutetea mijadala inayofaidi umma kwa jumla. 

Katika kanda ya Afrika Mashariki , Wizara ya Nchi za Kigeni huwa na mchango si haba katika kukuza matamanio ya mbunge ya kuongoza nchi wakati mmoja. Tom Mboya alijengwa vyema na Wizara hii kiasi cha kuonekana kuwa bora zaidi kumliko Rais mwenyewe Kitaifa na kimataifa. Kalonzo Musyoka alipoteuliwa kuwa Waziri katika wizara hii, ilimsaidia pakubwa kujijenga Kitaifa na Kimataifa kiasi kwamba hata serikali za mpito za Somalia naSudan zingali zinakumbuka juhudi zake za kuleta amani katika nchi hizi mbili. Si ajabu kutambua kwamba hii ndiyo sababu imempelekea kuwa na matamanio ya kuwania Urais ijapo 2007.  

  Nchini Tanzania, Jakaya Kikwete amekuwa Waziri wa nchi za kigeni kwa miaka 10 sasa. Kipindi hiki kilimpa nafasi ya kutambua ulimwengu tajriba ambayo ni muhimu kwa rais yeyote barani Afriika. Haikosi zaidi ya 80% ya Watanzania wamempa kura kuiongoza bongo.   Hii ina maana gani? Marais waliopo katika kanda ya Afrika Mashariki wanastahili kutambua siri hii. Kwamba tunawahitaji wao Wateue watu ambao wana uwezo wa kuwa Marais katika Wizara za nchi za Kigeni. Kwa njia hii, watawapa nafasi ya kutangamana na mataifa mengine ;tajriba ambayo itakuwa muhimu sana kwao endapo watakuwa Marais siku za usoni. Waziri kama huyu hastahili kuajiriwa leo na kufutwa kazi kesho kama ilivyo nchini Kenya. Hii ni kwa sababu huyu ndiye Afisa wa Uhusiano bora kati ya taifa na Ulimwengu kijumla. Haifurahishi kamwe kusikia kwamba leo Chirau Mwakere ametoa hotuba Marekani kama Waziri wa Nchi za Kigeni kish Kesho Raphael Tuju ndiye Waziri mpya wa nchi za kigeni.   Rais alioko mamlakani anastahili kumteua mtu msomi, anayependeka na wengi nchini kwa ajili ya kuzua sera na kuzitetea kitaifa na kimataifa. Sera zinazolenga kukwamua nchi kutokana na umaskini, sera zinazokweza nchi katika kiwango cha kimataifa. Waziri huyu anastahili kuwa msemaji hodari. Aielewe lugha ya Kiswahili, Kiingereza na lugha zingine za kimataifa. Awe mtu anayeielewa mifumo ya kiuchumi na sheria za kimataifa. Huyu ni mtu asiyestahili kuwa na mtazamo finyu wa maisha. Hastahili kuwa Mkabila na juhudi zake ndizo zinastahili kumzolea sifa kitaifa na katika ngazi za kimataifa.Hivyo basi Marais wa Kanda ya Afrika Mashariki hawastahili kuongozwa na ubinafsi katika kuwateua Mawaziri wa nchi za kigeni na wala hawastahili kuwaona waliwateua kama washindani katika kuwania Urais siku za usoni. Kwa njia hii, Rais atakuwa anajali maslahi ya nchi siku za usoni japo huenda yachukue muda.    Katika kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwajenga Marais wa siku zijazo. Licha kwamba Jakaya Kikwete alikuwa na nia ya kugombea Urais kitambo sana, haikumpelekea Rais Benjamin Mkapa kumwachisha kazi. Aidha sababu ya nyota ya Kikwete kung'aa wakati wa kampeni dhidi ya ile ya wapinzani wake ni kutokana na tajriba ya miaka 10 aliyoipata katika Wizara ya Nchi za Kigeni. Isitoshe Mkapa alijitokeza wazi kumuunga mkono Waziri wake tofauti na Rais mstaafu Daniel Moi aliyeamua kumuunga mkono kijana machachari badala ya aliyekuwa Waziri wa nchi za kigeni Mheshimiwa Kalonzo Musyoka.  Nchi ya Kenya kwa maoni yangu inakosa uhusiano mwema na jamii ya Kimataifa kutokana na kuyumbayumba kwa Wizara ya nchi za Kigeni. Licha ya Chirau Mwakwere kushtakiwa kuwa na uhusiano wa mahawara jijini Nairobi, Rais Kibaki alimteua Waziri wa nchi za kigeni na kumhamisha Kalonzo Musyoka. Kabla ya ubwabwa kumtoka Mwakwere shingoni amehamishwa na akateuliwa Raphael Tuju.     Raphael Tuju ni msemaji hodari; ndio sikatai. Ana elimu hasa tunapoelezwa kwamba aliisomea taaluma ya habari na ni Alumunae wa shule maarufu nchini ya Starehe. Kasoro yake ni kwamba Wakenya walio wengi wanamhusisha na vifo vilivyotokea Mkoani Nyanza. Hali ambayo inamfanya asipendeke hasa miongoni mwa jamii ya Waluo. Ana uwezo wa kuwa Waziri katika Wizara yoyote ile lakini si hii ya kumwakilisha Rais katika nchi za kigeni. Swali ni je Tuju akipewa miaka mingine 5 kama Waziri wa nchi za kigeni atakuwa na umaarufu na uwezo wa kuomba kura na kupewa na Wakenya walio wengi?    

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 2 Comments

ELIMU SIO MUHIMU NCHINI KENYA

Nchini
Kenya elimu si muhimu hata kidogo. Licha ya serikali kutumia fedha nyingi kuwaelimisha wanafunzi, wanafunzi hawa hawapewi nafasi ya kulijenga taifa kulingana na elimu waliyoipata. Hata uwe Professa mwenye digrii milioni moja hamna wa kutambua maarifa uliyo nayo angaa akupe nafasi ulikwamue taifa hili kutokana na tope la umaskini. Mfano ni Wangari Maathai ambaye juzi amepewa tuzo la kimataifa. Ole wake maanake Serikali ya Kibaki haitambui umaarufu wake na anachoweza kupata sasa ni unaibu wa waziri mbali si Uwaziri. 

  

Kuna binti hivi majuzi aliteuliwa kuwa mnaibu wa wizara ya vijana kisha akahamishwa mara moja hadi wizara isiyolingana na elimu yake. Nina uhakika Mbarire angetekeleza majukumu vizuri iwapo angeachwa pale maanake kipawa na elimu yake i pale.  

  

Yashangaza kusikia sekretari aliye na cheti pekee ndiye Waziri wa afya ilahali kuna wabunge jamani waliosomea Utabibu. Maina Kamanda ni naibu wa waziri pia licha kwamba elimu yake imepigiwa maswali. Kalembe ndile ni waziri wa utalii licha kwamba hana uwezo wa kuhamasisha ulimwengu kuhusu uhifadhi wa mazingira. Hata ingawa Prof Kivutha Kibwana ameisomea Sheria na uundaji wa katiba alichoweza kupata katika serikali hii ni uhifadhi wa miti. 

  

Tumearifiwa katika gazeti la Standard kwamba uteuzi wa Mabalozi unategemea unasaba wako na watu maarufu katika serikali. Aliteuliwa kakake Wilfred Machage, Kisha Mwakwere akamteua dadake, balozi mjini
Tokyo ni wa familia ya Moody Awori n.k. Uteuzi wa makatibu wa wizara vilevile si katika misingi ya elimu bali ni jinsi ulivyojiweka katika mtandao. Simeon Nyachae aliwaleta Wakisii kadhaa ambao wana unasaba, naye Musikari Kombo alikuwa ameapa kutokubali Uwaziri iwapo Waluhya hawatapewa nafasi kadha kama wakurugenzi wa mashirika ya serikali.  

  

Kiraitu Murungi alipokuwa Waziri wa Sheria amewaleta Wameru kibao katika wizara hii, swala ambalo huenda likampa kazi maradufu Waziri mpya Martha Karua.  

  

Haikosi hii ndiyo sababu wasomi wengi wasio katika mtandao wametorokea nchi za kigeni kutafuta ajira. Kumbuka wengi wa wasomi hawa walielimishwa kwa mikopo ya serikali na badala ya kupewa nafasi ya kufaidi umma kwa elimu waliyoipata serikali inawaajiri ndugu za mawaziri. Walio na elimu nchini Kenya ndio wanalisukuma taifa kwa kodi wanayotozwa licha ya mishahara
yao kuwa midogo. Mifano ya watu hawa ni walimu. Wasomi tuamkeni tudai haki yetu. Haiwezekani taifa kusonga mbele iwapo halitumii elimu ya raia wake na kuilipia elimu ile ipasavyo.  

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 1 Comment

SEHEMU ZA SIRI ZANYIMWA HAKI MAREKANI.

Haya ndiyo maendeleo wanayojivunia. Ya wanaume kuwa na uhusuano wa kimapenzi na wanaume wenzao. Yashangaza kuwaona wanawake wakikiuka kanuni za kimapenzi; kwamba sharti mwanamke aridhishwe kiu na mwanamume bali sio mwanamke mwenzake. Hii ndiyo demokrasia wanayoizungumzia na kuitangaza kote ulimwenguni. Dhambi ya aina hii imeambukizwa vijana pia huku Marekani na huwezi katu kuwakaripia maanake sheria za nchi zinalinda demokrasia,
kama wanavyosema. Unapotazama filamu zao mojawepo ya maudhui ni ngono za jinsia moja.  

  Inapotukia ngono kati ya mwanamume na mwanamke, mambo yanakuwa ya firauni sasa. Midomo imechukua nafasi ya sehemu za siri ya mwanamke na mwanamume.Yashangaza kusikia jinsi hawa 'walioendelea' ni wachafu hasa katika midomo
yao. Mbona mwanamke anyonye shakawa za mwanamume huku mwanamume akipata uhondo katiba kukiramba kile kidude. Ikizidi wataziramba ngoko pia; kunakotokea kinyesi. Nimekuwa makini sana kutompa busu yeyote hapa Marekani maanake sijui dakika chache zilzopita alikuwa akifanya kazi gani na siko tayari kupakwa kinyesi katika shavu langu mie.  

  Kuna msamiati huku kwa jina sherehe za kimapenzi au kwa king'eng'e wanaziita 'sex parties'. Hapa swala kuu si kuonja vyakula mbalimbali vilivyotayarishwa bali ni kumuonja yeyote yule aliyekuja. Hamna faragha hapa. Ngono zitafanywa wazi sakafuni, kutani, vitandani kwenye makochi n.k. Juzi kumekuwa sherehe hapa chuoni Brown. Waliita sherehe
yao 'Gay Students Association'. Ili uweze kukubalika, ulihitajika kuja pale ukiwa uchi au chupi na kanchiri pekee. Nilikuwa pale kushuhudia jinsi 'demokrasia' imekengeusha wanafunzi Wamarekani.  

  Usimwone binti na ghulamu wamekubatiana ukadhani itakuwa hivi hadi kifo kitakapowatenganisha. Jana binti huyu alikuwa na boifrendi tofauti na juzi na atakuwa tofauti pia ijapo kesho kutwa. Katika ndoa ni vivyo hivyo. Iwapo mwanamume ameanza kulegea basi huenda akaletewa ndume kazi kitandani mwake. Katika matangazo yao utaona tangazo
kama hili;  

               

             "Mimi na mume wangu tumeamua kuwa na mhusika wa tatu katika ngono. Ningependa   

              kumtazama mume wangu akifanya ngono na mwanamke mwingine…."    

Mniambie Wakristo nikidhani pia Waislamu, je haya yanakubalika katika dini? Licha kwamba wenzetu hawa ni matajiri wa tekinolojia wao ni maskini hohehahe wa kimaadili. Nina uhakika bara la Afrika ndilo linaongoza ulimwenguNI katika kuwa na utajiri mkubwa wa maadili ya jamii.   

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 9 Comments

WAMAREKANI WANAVYOMTHAMINI MBWA.

 

 

            Tofauti na wakenya walio wengi, kwa Wamarekani mbwa ni almasi iwapo si dhahabu. Huyu ni kiumbe aishiye kwenye makasri na wanadamu huku Marekani. Akiwa ndani ya kasri basi mbwa huyu ana haki ya kuingia chumba chochote atakacho pasi kubisha hodi. Haijalishi chumba atakamoingia mbwa atampata mwenye nyumba akiwa uchi au la. Waama mbwa wa kiafrika atamwonea gere mbwa wa kimarekani kwa jinsi ambavyo mbwa huyu analelewa kwa utashi.

            Ni nadra kumpata mkenya akimpa busu mbwa. Wamarekani swala hili si hoja. Nikidhani mwenye mbwa atampa mbwa wake busu la kukata na shoka kuliko jinsi atampa mpenziye. Kwetu sisi hatuwabusu mbwa mbali tunavitupilia mbali vyombo alivyonusanusa mbwa huyu.

            Ukija Marekani ndugu utashuhudia haya bila shaka. Mabwana na mabibi wakiwa ziarani na mbwa wao hawasahau kubeba mikoba ya kuokotea vinyesi vya mbwa. Mwenye mbwa yu macho kutizama mbwa wake atakapochutama. Mara moja atatoka mbio kama mshale kwenda kuokota kinyesi na kukitia mkobani. Eti wanjali mazingira! Kwetu sisi harufu ya kinyesi cha mbwa itaweka makunyugu pua zetu na kutufunga macho kwa ghafla angalau tusikione kinyesi.

            Waama mbwa nchini marekani wana bajeti kubwa yakhe! Nina uhakika kiasi cha fedha kitumiwacho kwa mbwa nchini Marekani kila mwaka chatosha kulikwamua bara la Afrika kutoka katika lindi la umaskini. Mbwa atalishwa kwa chakula kilichosawazishwa, atakingwa kutokana na maradhi, atakuwa na yaya wa kumlinda nyumbani miongoni mwa matilaba mengine.

            Waliotazama janga la kibunga cha Katrina mtakubaliana nami kwamba ilkuwa heri mbwa kuokolewa kwanza kisha tuanze kutafuta binadamu alipo. Mbwa wengi waliokolewa kutoka vyomba vilivyokuwa vimesombwa huku watu wakifa maji.

            Iwapo bwana enda safari na mbwa wake na iwe kwamba atatumia gari basi mbwa atakuwa na kiti chake spesheli. Ole wako mkenya uliozoea kuomba lifti. Samahani maanake kiti kishakaliwa tayari na mbwa! Ukipenda basi jisombe nyuma palipo mizigo na katu usitatize starehe za mbwa wangu. Ikizidi vilevile, usimtamzame mbwa wangu kwa jicho la dharau maanake nitakufungulia mashtaka kortini.

            Visa vingi kortini ni vya huyu kamwiba mbwa wangu, yule alimtisha mbwa wangu, huyo hampendi mbwa wangu n.k. Mbwa ni msamiati wa kila mara bongoni mwa Mahakimu na Viongozi wa mashtaka. Mbwa angekuwa na uwezo wa kujitetea angetiwa vizibani kujitetea huku Marekani.

            Amini usiamini huku Marekani talaka ni jambo la kawaida. Ndoa huku ni kandarasi. Nikichoshwa na yako mapenzi nenda potelea mbali! Uniache na mbwa wangu. Imekuwa heri kwao kuishi na mbwa kuliko kuishi na libaba lililioshiwa na nguvu za kiume. Nadhani mbwa angekuwa na uwezo wa kufanya mapenzi na binadamu basi ungempata vitandani na wake au waume za watu wakizicheza.

                        Mambo yalivyo huku ndugu ni kwamba wamarekani wanampa mbwa nafasi ilyovuka mipaka. Ni sawa siwapingi lakini inapofikia kiwango cha kutojali binadamu mwenzako, mpenzio n.k basi nafikiri huku ni kukengeuka. Jumapili baadhi yao hawendi kumwabudu mwenyezi MUNGU aliyewapa hao mbwa. Badala yake huwa ni nafasi nzuri ya kuwatembeza mbwa wao. Mambo Mbotela, unambie leo, huu ni uungwana?

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet

BIASHARA YA ELIMU: TUIGE MAREKANI

Ukweli ni kwamba popote walipo Marekani sharti wawe na lengo la kupata faida. Iwapo sivyo, watafunganya virago na kuondoka. Nchi hii imejiendeleza katika kila hali kwa kuwekeza mtaji katika biashara za kilimwengu. Kila taasisi Marekani imeajiri wataalam wa biashara kwa lengo la kupata maarifa ya jinsi ya kufanya biashara. 

  

Baadhi ya biashara ambazo Marekani wamefanikiwa ni biashara ya uhamiaji, biashara ya shule za kimataifa katika nchi geni, biashara ya mitihani k.v. TOEFL, SAT, GRE , biashara ya kutoa mikopo kwa mataifa maskini n.k. Vyuo vikuu vimechangia pakubwa pia katika kuujenga uchumi wa Marekani.  

  

Katika makala hii nitafafanua jinsi vyuo vikuu vinafanikisha biashara za Wamarekani. Vyuo hivi hutangaza nafasi kwa walimwengu bali sio kwa Wamarekani pekee. Wamefanikiwa kufanya hivi kwa kuweka vyuo hivi vyote katika mtandao kiasi kwamba mwenye kiu ya elimu atapata habari kuvihusu kwa urahisi. Iwapo wewe si Mmarekani utahitajika kufanya mitihani kadha ili uweze kukubalika. Mtihani maarufu ni ni TOEFL ambao haujali iwapo kama ulifunzwa Kiingereza na malkia
Elizabeth mwenyewe. Mitihani hii inaizalishia Marekani mabiliono ya pesa kutoka kote ulimwenguni. 

  

Ukishapasi TOEFL, mambo bado; utahitajika kulipa fedha za usajili chuoni zisizorudishwa. Vyuo vingi vitatoza kati ya Dola 50 na 100. Nitawapa mfano wa chuo kikuu cha Brown. Waliotuma maombi ya usajili mwaka huu walikuwa takribani 17,000. Hawa wametoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Hivyo basi ina maana kwamba chuo kilikusanya shilingi milioni 8,568,000 za
Kenya. Miongoni mwa hawa 17,000 ni 2,400 waliokubaliwa kujiunga na chuo. Hii ina maana kwamba 14,600 hawakubahatika licha kwamba washalipa shilingi 5,040 kila mmoja. Wengi wa hawa wasiokubaliwa ni wa kutoka nchi za kigeni. 

  

Pesa hizi na pamoja na karo inayolipwa na waliofanikiwa, ndizo hutumika kulipa mishahara ya Wahadhiri na wafanyikazi wengine Chuoni. Kwa njia hii vyuo hivi havitegemei kamwe pesa zozote kutoka kwa serikali. 

  

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet

USAWA WA MWANAMKE NA MWANAMUME: MADHARA YAKE

Nchi yetu ya
Kenya imetambulika kukumbatia maswala ibuka ya kilimwengu pasi kupigia maswali madhara yake. Aghalabu badhi ya maswala haya yameibuka katika mataifa ya magharibi kisha yakaenezwa kwa lazima ama kwa hiari katika mataifa yanayoendelea. Mifano ya maswala haya ni Usawa wa kijinsia, demokrasia, kutoadhibiwa kwa mtoto n.k. 

  

Usawa wa kijinsia ni ile hali ya mwanamke kufanywa sawa na mwanamme licha ya tofauti zao za kibaolojia. Katika mhemko huu wa kilimwengu, mwanamke hukakania kudai kwamba chochote awezacho kufanya mwanamume ,mwanamke pia aweza. Labda lililobaki ni mwanamume kutiwa ujauzito na mwanamke. Kwamba kielimu, kifamilia,kisiasa,kidini, kiuchumi, mwanamke anaweza kufanya
kama au bora zaidi ya mwanamume. Katika siasa Ngilu,maathai,Karua,Nyiva,Ndetei,Mugo na wengine wamedhihirishia bara hili na ulimwengu kijumla kwamba mwanamke ni sawa na mwanamume. 

  

Lakini swali ni je usawa huu una madhara yepi kufikia sasa? Nchini Marekani mwanamke amejichukuliwa sawa na mwanamume kiasi ya kwamba atakuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa. Hali hii imepelekea wanawake kuuawa ovyo na waume zao nchini Marekani. Pili ndoa zinavunjika kila wakati Marekani na imekuwa kawaida sasa. Wote ni vichwa katika familia na mwanamke katu hakubali nafasi aliyopewa na dini ya Kikristo kwamba atakuwa msaidizi wa mwanamume. Talaka imekuwa msamiati wa kutamkwa hata na mtoto mchanga Marekani. Hivi sasa idadi ya wanawake waliotalikiana na waume zao Marekani inazidi kuongezeka. Wanawake kama hawa aghalabu huwa hawana nafasi nzuri zaidi ya kujipatia waume wengine maanake wamezeeka. Mwanamume kigogoyo kwa kiasi kikubwa atapata kibinti kirembo hata baada ya kutalikiana na mkewe.  

  

Katika sekta ya uajiri wanawake wamedai nafasi sawa pia. Ukweli ni kwamba hata ofisi iwe na wanawake kiasi gani kuna kazi ambazo watahitaji msaada wa wanaume. Hapa chuoni Brown, sera ya uajiri sawa wa wanawake na wanaume imeleta hasara badala ya faida. Mfano ni ofisi ya usajili amabayo asilimia kubwa ya wafanyikazi ni wanawake. Kazi kama vile za kuinua vitu vizito na kwenda kupokea barua posta imelazimu waajiri wanaume wa muda. Kumbuka ilidhaniwa kwamba wanawake hawa watafanya kazi zote hizi lakini wapi.  

  

Nchini
Kenya wengi wanaojiita watetezi wa haki za mwanamke wametalikiwa na waume zao pia. Sitataja majina kwa usalama wangu na wao. Wanaume ulimwengu mzima wana tabia sawa kwa kiasi kikubwa dada zangu. Hawataki ushindani katika familia. Wanaona fahari kuwa wakurugenzi wa familia zao na kamwe hawatarajii wake zao kujilimbikizia hadhi hii hata wanapokuwa maiti kaburini. Mwanamke anayetazamia mumewe aingie jikoni apike kisha aingie dobi na kufua nguo anajidanganya.  Wengi wa watetezi wa haki za mwanamke wamejipata katika visiwa vyao pekee, bila wa kumwita mpenzi karibu. Wengi wameishia mahakamani kushtaki wake wenza kwamba wamewaiba waume zao. Kasoro ni nyie kutaka nafasi za waume zenu.  

  

Watoto wanapokua, wanaanza kudai baba zao. Hawako tayari kujisajili shuleni kwa majina ya mama zao eti David Wambui, au Peter Adhiambo. Swala hili linawapa tumbo joto wanawake waliotalikiwa na waume zao kwa kudai usawa nyumbani.  Vitoto vya kike vilivyoambukizwa ugonjwa huu wa usawa wa mwanamke vinaishia kuona ya Firauni. Licha ya wavulana kuwaahidi paradiso hapa duniani, vibinti hivi vinaishia kutumiwa kimapenzi tu kisha waume wasiokubali usawa wanaishia kuoa wanawake wanyenyekevu.  

  

Maswala kama haya miongoni mwa mengine yanastahili kutiliwa maanani na wanawake kabla ya kubugia mihemko ya magharibi kikondoo. 

  

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet

U.N. INAVYOFILISISHA MATAIFA MASKINI.

U.N. INAVYOFILISISHA MATAIFA MASKINI. 

Unaposikia shirika lisilo la kiserikali limo nchini kusaidia maskini, wakimbizi, wanaougua n.k. unastahili kujua kwamba wanatumia fedha za ulimwengu kufanya hivi bali sio fedha za mataifa
yao mahususi. Umoja wa mataifa(U.N.) ni mvuto wa rasilimali kutoka mataifa mbalimbali.Umuhimu wa  Rasilimali hizi ni kutatua majanga ya kilimwengu ili ulimwengu uwe pahali pema zaidi pa kuishi. Baadhi ya majanga haya ni usalama, magonjwa, Ukimbizi, umaskini, uchafuzi wa mazingira n.k. 

  

Panapotokea janga fulani ulimwenguni wadau wengi huwa mbioni kuandika miswada itakayowawezesha kupata hela kutoka U.N. kusudi waweze kujifaidi na kutatua janga lile. Kwa mfano iwapo Somalia imeingiwa na vita kisha wananchi wake wakatorokea
Kenya basi inakuwa faida kwa baadhi ya watu na mashirika yanayopokea misaada kutoka UN. Hii ndiyo sababu tuna mashirika kama vile Care International. Action AID, German Technical Coperation n.k. 

  

Tunapochunguza kwa jicho pevu swala hili la UN na ugawaji utajiri wa kilimwengu utagundua kwamba wanaofaidi ni mataifa ya magharibi. Mashirika mengi yanayodai kutatua majanga ya kilimwengu ni ya bara Uropa au Marekani. Hii ina maana gani? Utajiri uliovutwa kutoka ulimwengu mzima unafaidi upande mmoja. Kuwepo Koffi Annan
kama katibu wa shirika hili ni kifumba macho tu. Ni namna ya kutufurahisha sisi Waafrika pamoja na bara Asia kwamba Kiongozi wa UN ni Mwafrika.  

  

Nikitumia mfano wa CARE INTERNATIONAL (RAP) ambalo ni shirika linaloshughulikia wakimbizi katika kambi za wakimbizi Daadab na Kakuma nchini
Kenya. Wadau wa shirika hili wanatoka nchini CANADA. Wanawatumia Wakenya wachache kupokea misaada kutoka UNHCR. Kazi ya Marangu ambaye ni mmoja wa Meneja katika kambi ya Daadab ni kuandika miswada. Akisha maliza anawapokeza wenye hisa katika kampuni hii ya Care International ili waweze kupokea misaada. Wenye hisa nao wanaikabidhi UNHCR ambalo ni tawi la UN. Dola zikishatoka, basi wenye hisa wanatoa kiasi chao kisha wanatoa kiasi kingine ni cha kuwalipa wafanyikazi na kuendesha ofisi zao Nairobi. Kiasi kinachobaki ndicho kitawafaidi wakimbizi. 

  

Silaumu mashirika ya mrengo wa kushoto kufanya biashara na UN. Linaloniumiza ni eti hamna Mashirika yanayomilikiwa na Waafrika wenyewe ili waweze kufaidi kutokana na utajiri huu wa UN licha kwamba mataifa ya Afrika ni washika dau katika UN.Sina habari iwapo Waafrika wanajiona duni kumiliki mashirika
kama haya au wananyimwa nafasi ya kushiriki katika biashara hii. Nikiamini vilevile licha kwamba Koffi Annan ndiye kiongozi wa UN walio chini yake wengi ni wa mataifa ya magharibi. Hivyo basi Mashirika ya magharibi yanapopokeza miswada yao inakuwa raisi kwao kupokea misaada.  

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | No Comments Yet

UISLAMU HAUWAPI UHURU WAISLAMU.

UISLAMU HAUWAPI UHURU WAISLAMU. 

  Ninakubaliana na Waislamu katika maswala mengi yanayojenga utamaduni wa Waislamu. Mfano ni namna wanawake wanavyovalia, na jinsi mwanamume amepewa nafasi ya juu katika maswala ya dini tofauti na mwanamke. Vilevile natamani namna ambavyo wamejitolea kusali mara tano kwa siku. Na zaidi ni jinsi walivyo wakarimu katika kutoa zaka zao zinazowasaidia wasiojiweza katika jamii. 

  Mojawepo ya mambo nisiyokubaliana nao ni jinsi ambavyo dini hii haiwapi uhuru wafuasi wake kuchagua wanalopenda. Ni kweli kwamba kuna baadhi ya Waislamu ambao wamechoshwa na dini ya Kiislamu na sasa wanataka kubadili wawe Wakristo, Wabudha, Wahindi n.k. Ni kweli kwamba kuna mabinti waislamu ambao wamewavutia wanaume wasio waislamu lakini hawawezi kukubali kuolewa nao kwa sababu Uislamu hauruhusu hivyo. 

  Aidha mwanamume anapovutiwa na binti wa Kiislamu anastahili kuslimu kwanza ili aweze kukubalika na binti na jamaa yake. Inapotokea kwamba binti wa Kiislamu ameamua kuolewa na ghulamu asiye Muislamu basi inakuwa balaa. Na inapotukia kwamba Muislamu ameibadili dini yake na kuwa Mkristo basi Sharia yasema, adhabu ya kosa
kama hili ni kifo.  

  Yalitukia Afghanstan jana; mwanamume kwa jina Abdul Rahman alifikishwa mahakamani kwa kosa la kubadili dini na kuwa Mkristo. Waafghanistani walio wengi wanataka auliwe maanake ametenda kosa lisiloweza kusamehewa. Mataifa ya magharibi nayo pamoja na wanaopenda demokrasia kote ulimwenguni wamekuwa wakili wa bwana huyu ambaye sasa anakiri Yesu Kristo kuwa mwana wa MUNGU aliyekufa kwa ajili ya dhambi zake.  

  Miezi iliyopita kulikuwa na mwito wa Waislamu kote ulimwenguni kususia bidhaa na uhusuano wao na nchi ya
Finland kwa sababu kulikuwa machapisho ya vibonzo vya Mohammed. Walimwengu walishuhudia hasira za Waislamu kote ulimwenguni. Kulikuwa na uteketezwaji wa balozi za Finland na kutokuwepo usalama katika baadhi ya miji mikuu ya ulimwengu. Nilipowashauri baadhi ya marafiki zangu Waislamu kwamba wanastahili kusali ili MUNGU awasamehe hawa wachapishaji wa vibonzo walikataa katakata. Walisema Uislamu unaamini kutenda. Hivyo basi una fununu cha walichodhamiria kutenda.  

  Maoni yangu ni kwamba Waislamu wanastahili kutambua kwamba tunaishi katika ulimwengu unaobadilika kila wakati. Yesu Kristo mwenyewe alitofautiana mara nyingi na wafarisayo kwa sababu ya sheria za Musa. Alipomponya mgonjwa siku ya sabato waliteta kwamba ni kinyume cha sheria za Musa. Mwanamke kahaba alipoletwa mbele zake alimwacha huru tofauti na nia
yao Wafarisayo kwamba alistahili kuuliwa.  

   Iwapo Muislamu ameamua kubadili dini basi na iwe hivyo. Ni haki yake. Haistahili kuwekewa adhabu ya kuuawa. Wanalostahili kufanya Waislamu ni kumuhubiria pasipo kumshurutisha. Hivi ndivyo Ukristo ulivyo. Akiamua Mkristo kuwa Mubudha hatahukumiwa kifo bali Wakristo watajitolea kumuhubiria kwa upendo angalau aweze kubadili nia. Akiwa sugu basi Mkristo atafunga na kumwombea huyu ili MWENYEZI MUNGU amtendee miujiza. Dini ya kikweli ni ushirika kati ya MUNGU na mshirika eti. Hukumu ya MUNGU kwa wanaoiasi dini ni muhimu zaidi kuliko hukumu ya binadamu.      

March 27, 2006 Posted by Daudi Kyeu | Uncategorized | | 2 Comments