MIAKA 14: UMRI WA MTOTO KUFANYA KAZI MAREKANI.
Iwapo serikali za bara Afrika zina lengo la kupunguza umaskini, ipo haja ya kuhakiki baadhi ya sheria ambazo hazina mantiki kamwe. Nchini Kenya kwa mfano, raia wamelazimishwa kuamini kwamba ni kinyume cha sheria kumwajiri mtoto akiwa na umri wa chini ya miaka 18. Kwa king'eng'e wanaiita hali hii 'child labor'.
Kutowatambulisha watoto katika ulimwengu wa kazi kumewafanya kuwa wazembe kiasi cha kununuliwa chupi na mama zao. Nina maana ya watoto walio kati ya umri wa miaka 14-18. Hali hii imepelekea wazazi kutumia rasilimali nyingi kwa watoto kiasi cha kusahau kujali maslahi yao pia. Chukulia kwa mfano mzazi aliye na watoto wanne walio kati ya miaka 14 na 18. Kisha mzazi huyu mshahara wake ni dola 100 kwa mwezi. Mzazi hataweza kuwakidhia watoto hawa mahitaji kwa ubora unaohitajika.Watoto hawa wana umri tosha wa kwenda kusaka kazi hata kama ni ya uyaya au kuosha vyoo. Mradi wapate fedha za kukidhia mahitaji yao.
Nchini Marekani umri wa mtoto kufanya kazi ni miaka 14. Wengi wa watoto walio na umri huu ni wa shule za upili. Baada ya shule jioni, watoto hawa hujitoma katika soko la kazi kutafuta dola. Utawapata wakiosha vyombo katika hoteli, wakifanya uyaya wa muda au kuwatembeza mbwa wa jamaa fulani. Wao hufanya kazi kwa muda kabla ya kwenda nyumbani kufanya mazoezi waliyopewa shuleni. Tajriba hii anayopata mtoto wa Kimarekani humwongezea sifa katika kapu lake siku za usoni atakapotazamia kutafuta kazi ya kudumu.
Nchini Kenya, vitoto vingi hata vyenye umri wa zaidi ya miaka 20 hutarajia wazazi wao kuwakidhia kila takwa. Wanaponing'onozewa kwamba hoteli fulani inahitaji mfanyikazi wa muda vitoto hivi huona hii ni kazi ya wasio na elimu. Itakuwa heri kwao kucheza basketi boli, au kutazama runinga kisha jioni wende nyumbani kuandaliwa chakula.
UHAKIKI WA WAGOMBEA 4 WA URAIS 2007 NCHINI KENYA.
Walio na hamu ya kuwa rais nchini Kenya wameanza kujinadi sasa. Kila mmoja anajaribu kupiga zumari isikike nje ya eneo lake la uwakishi bunge. Hadi kufikia jana dalili inaonyesha kwamba wanaotaka kupokea mshahara wa zaidi ya milioni mbili kila mwezi wamejikita katika makundi mawili ya kisiasa. ODM na NARC KENYA. Washika dau wakuu katika ODM(Orange Democratic Movement) ni LDP na KANU. Kisha NARC Kenya imeanza kuvutia mabaki ya muungano wa awali(NARC) na baadhi ya vyama vingine kama vile DP. Inadaiwa kwamba Rais Kibaki yuko katika NARC KENYA hata ingawa hajatangaza rasmi. Hata hivyo miongoni mwa wale wanaogombea urais 2007 kunao wanne ambao raia kote nchini wamejinasibisha nao. Hawa ni Mwai Kibaki , Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Uhuru Kenyatta.
KIBAKI
Ana uzamili( Masters) katika maswala ya Kiuchumi kutoka Makerere. Amekuwa makamu wa rais miaka ya 80 kabla ya kuwa waziri wa fedha miaka ya 70. Amekuwa kiongozi rasmi wa upinzani baada ya kujiuzulu kutoka KANU. Ana umri wa zaidi ya miaka 70. Anatokea katika jamii ya Wakikuyu ambao ndio wengi nchini Kenya. Hivi sasa ni rais wa Kenya. Amekuwa mbunge Nairobi kabla ya kuhamia nyumbani. Ana zaidi ya miaka 30 katika siasa. Ni mkatoliki. Haijulikani iwapo yuko NARC au ni NARC KENYA.
KALONZO MUSYOKA
Ana shahada katika sheria kutoka Nairobi. Amekuwa waziri wa nchi za kigeni katika serikali ya KANU. Amekuwa waziri katika wizara zaidi ya nne katika maisha yake ya uanasiasa. Wiizara zenyewe ni Utalii, Elimu, Mazingira Utalii n.k. Ana umri wa kati ya 52 na 55. Amekuwa mwanasiasa mwaminifu katika enzi ya KANU. Hajahusishwa na kashfa zozote zile za ufisadi. Amekuwa mhakiki katika serikali ya Kibaki hali iliyopelekea yeye kuachishwa kazi kama waziri. Ana zaidi ya miaka 20 katika siasa. Amekuwa mstari wa mbele kufanikisha amani Sudan na Somalia. Hivi sasa yuko katika LDP, tawi la ODM. Anatokea katika jamii ya Wakamba mkoa wa Mashariki.
RAILA ODINGA.
Ana uzamili katika Uhandisi kutoka Ujerumani. Amekuwa katika upinzani tangia alipoingia katika siasa. Hata hivyo amekuwa serikali ya KANU kwa muda mfupi na vile vile katika serikali ya Kibaki. Ana uwezo wa kuvuta umati kwa namna anavyotumia lugha. Ni mbunge Nairobi licha kwamba anaathiri pakubwa siasa mkoani Nyanza anakotokea. Ametiwa korokoroni kwa msimamo wake sugu wa kisiasa katika miaka ya 80. Ana umri wa miaka 60. Amekuwa waziri wa ujenzi wa barabara kabla ya kutimuliwa kutoka katika serikali ya Kibaki. Kiwanda wanachomiliki kama familia kimetajwa katika uchunguzi wa ufisadi nchini. Yuko katika LDP tawi la ODM
UHURU KENYATTA.
Amelelewa kwa utashi tangu alipotungwa tumboni mwa mamaye. Babake alikuwa mwanzilishi wa taifa. Ana digrii ya siasa na uchumi kutoka Marekani. Amekuwa Marekani kwa muda mrefu kabla ya kuja nyumbani kupokea uongozi wa KANU kutoka kwa Daniel Moi. Ana umri wa kati ya miaka 43 na 48. Ana biashara kibao. Amegombe ubunge wakati fulani na kuukosa hadi alipopendekezwa kugombea urais. Anatokea katika jamii ya wakikuyu mkoa wa kati. Hivi sasa ni kiongozi rasmi wa upinzani. Aliongoza msafara hadi Uingereza kumuhoji aliyekuwa katibu wa maadili kuhusu kashfa ya Anglo Leasing( ufisadi katika serikali ya kibaki). Yuko katika KANU tawi la ODM
GHARAMA YA KUCHAGUA RAIS MPYA KILA BAADA YA MIAKA 5.
Hata ingawa wananchi nchini Kenya watachangamkia kuchagua rais mpya kila baada ya miaka 5, kuna gharama fiche ambayo raia hawajaitambua. Nchini Kenya tumewastaafisha marais wawili sasa; Jommo Kenyatta na Daniel Moi.
Rais anapostaafu ina maana kwamba anastahili kupokea marupurupu ya uzeeni. Nikirejelea mfano wa Mstaafu Daniel Moi, marupurupu aliyopokea ni mengi sana. Tukianza na maelfu ya pesa anazopokea kila mwezi, kisha ulinzi na magari yanayotiwa mafuta, kuendeshwa na kurekebishwa kwa ushuru unaotozwa wananchi. Hali ni vivyo hivyo nyumbani kwa Jommo Kenyatta.
Tuchukulie kwa mfano, Kibaki atashindwa katika uchaguzi ujao, atakuwa ametumikia nchi kwa miaka 5. Tuchukulie pia atakayetwaa mamlaka atashindwa katika uchaguzi wa 2012. Iwapo hali itakuwa hivyo kwa kipindi cha miaka 20 ina maana kwamba tutakuwa na marais 6 wanaopokea marupurupu kutoka katika ushuru unaotozwa raia.
Marupurupu wanayopewa marais wastaafu nchini Kenya ni mengi. Na mtindo kama huu ni wa kufilisisha umma badala ya kuwahudumia. Maoni yangu ni kwamba rais anastahili kupewa nafasi ya miaka 10 kuongoza nchi. Iwapo wananchi wameridhishwa na uongozi wake basi anaweza kugombea urais zaidi na zaidi.
Hata ingawa uongozi wa Moi kwa miaka 24 uliandamana na ufisadi, kwa kiasi fulani haukupelekea kunyonywa kwa mfuko wa umma kwa misingi eti marupurupu ya rais anayestaafu. Tungebadili rais kila baada ya miaka 5 katika kipindi hiki Moi alikuwa mamlakani ina maana kwamba hivi sasa tungekuwa na marais 6 wanaopokea marupurupu kutoka kwa mfuko wa umma.
Nikidhani hii ndiyo sababu ya baadhi ya mataifa kudumisha uongozi wa kifalme. Hii ni kwa sababu kuna familia moja tu iliyo mamlakani, hivyo basi matumizi ya fedha za umma yanakuwa machache kuliko mataifa yanayobadili rais kila baada ya muda fulani.
Kwa misingi hii ya kiuchumi basi Kibaki anastahili kupewa miaka mingine 5 uongozini. Kazi yake ikiwa nzuri mwishoni na awe na hamu ya kugombea tena basi wananchi wanastahili kumpa kura.
KENGEN YAUZA HISA SASA.
Ndugu zangu Wakenya wana habari kwamba KENGEN( Shirika pweke la usambazaji umeme Kenya) inauza 30% ya hisa zake kwa umma. Kwa Wakenya ni shilingi 11.90 za Kenya kisha kuna bei ya raia kutoka TZ na Uganda ambayo ni nafuu kiasi kuliko ya wageni kutoka nchi zingine.
KENGEN ni mojawepo ya mashirika ambayo hadi sasa yanamilikiwa na serikali. Historia inaonyesha kwamba KENGEN imekuwa ikipata faida tangu ilipoanzishwa. Hii ni mara ya kwanza tangu Kenya kupata uhuru Serikali kujaribu kuwapunguzia raia umaskini kwa kuweka mazingira mufti ya uwekezaji.
Hisa zimeanza kuuzwa tarehe 20 machi na itafungwa tarehe 14 Aprili. Panapo majaliwa huenda mwisho wa mwaka thamana ya hisa hizi itakuwa imepanda hadi kufikia zaidi ya shilingi 50 za Kenya. Hivyo itakuwa faida kwa yeyote ambaye atakuwa amewekeza.
Kwa WaTZ mnaweza kuwatuma jamaa zenu Kenya katika Kenya Commercial Banks ili waweze kuwanunulia hisa kabla ya kipindi kufungwa. Iwapo mtahitaji habari na usaidizi zaidi niko tayari kuwapa maanake tunaelekea kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
WIZARA YA NCHI ZA KIGENI AFRIKA MASHARIKI.
Nchi zilizoendelea zimejua kutambua vipawa vya wanasiasa wakiwa wangali vijana. Katika hali hii kipawa cha mwanasiasa kinapotambulika, yeye huwekwa katika mazingira ambamo yatamsaidia kukuza kipawa kile ili labda siku za usoni aweze kufaidi nchi akiwa na tajriba toshelevu. Nchini Marekani kwa mfano, chama cha upinzani kimetambua kipawa cha Barrack Obama; na inasemekana kwamba licha ya yeye kuwa Mmarekani mweusi, ana nafasi nzuri hata ya kuwania Urais siku za usoni. Hivyo basi ,amekuwa malighafi ya kutegemewa katika kuzua na kutetea mijadala inayofaidi umma kwa jumla.
Katika kanda ya Afrika Mashariki , Wizara ya Nchi za Kigeni huwa na mchango si haba katika kukuza matamanio ya mbunge ya kuongoza nchi wakati mmoja. Tom Mboya alijengwa vyema na Wizara hii kiasi cha kuonekana kuwa bora zaidi kumliko Rais mwenyewe Kitaifa na kimataifa. Kalonzo Musyoka alipoteuliwa kuwa Waziri katika wizara hii, ilimsaidia pakubwa kujijenga Kitaifa na Kimataifa kiasi kwamba hata serikali za mpito za Somalia naSudan zingali zinakumbuka juhudi zake za kuleta amani katika nchi hizi mbili. Si ajabu kutambua kwamba hii ndiyo sababu imempelekea kuwa na matamanio ya kuwania Urais ijapo 2007.
Nchini Tanzania, Jakaya Kikwete amekuwa Waziri wa nchi za kigeni kwa miaka 10 sasa. Kipindi hiki kilimpa nafasi ya kutambua ulimwengu tajriba ambayo ni muhimu kwa rais yeyote barani Afriika. Haikosi zaidi ya 80% ya Watanzania wamempa kura kuiongoza bongo. Hii ina maana gani? Marais waliopo katika kanda ya Afrika Mashariki wanastahili kutambua siri hii. Kwamba tunawahitaji wao Wateue watu ambao wana uwezo wa kuwa Marais katika Wizara za nchi za Kigeni. Kwa njia hii, watawapa nafasi ya kutangamana na mataifa mengine ;tajriba ambayo itakuwa muhimu sana kwao endapo watakuwa Marais siku za usoni. Waziri kama huyu hastahili kuajiriwa leo na kufutwa kazi kesho kama ilivyo nchini Kenya. Hii ni kwa sababu huyu ndiye Afisa wa Uhusiano bora kati ya taifa na Ulimwengu kijumla. Haifurahishi kamwe kusikia kwamba leo Chirau Mwakere ametoa hotuba Marekani kama Waziri wa Nchi za Kigeni kish Kesho Raphael Tuju ndiye Waziri mpya wa nchi za kigeni. Rais alioko mamlakani anastahili kumteua mtu msomi, anayependeka na wengi nchini kwa ajili ya kuzua sera na kuzitetea kitaifa na kimataifa. Sera zinazolenga kukwamua nchi kutokana na umaskini, sera zinazokweza nchi katika kiwango cha kimataifa. Waziri huyu anastahili kuwa msemaji hodari. Aielewe lugha ya Kiswahili, Kiingereza na lugha zingine za kimataifa. Awe mtu anayeielewa mifumo ya kiuchumi na sheria za kimataifa. Huyu ni mtu asiyestahili kuwa na mtazamo finyu wa maisha. Hastahili kuwa Mkabila na juhudi zake ndizo zinastahili kumzolea sifa kitaifa na katika ngazi za kimataifa.Hivyo basi Marais wa Kanda ya Afrika Mashariki hawastahili kuongozwa na ubinafsi katika kuwateua Mawaziri wa nchi za kigeni na wala hawastahili kuwaona waliwateua kama washindani katika kuwania Urais siku za usoni. Kwa njia hii, Rais atakuwa anajali maslahi ya nchi siku za usoni japo huenda yachukue muda. Katika kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwajenga Marais wa siku zijazo. Licha kwamba Jakaya Kikwete alikuwa na nia ya kugombea Urais kitambo sana, haikumpelekea Rais Benjamin Mkapa kumwachisha kazi. Aidha sababu ya nyota ya Kikwete kung'aa wakati wa kampeni dhidi ya ile ya wapinzani wake ni kutokana na tajriba ya miaka 10 aliyoipata katika Wizara ya Nchi za Kigeni. Isitoshe Mkapa alijitokeza wazi kumuunga mkono Waziri wake tofauti na Rais mstaafu Daniel Moi aliyeamua kumuunga mkono kijana machachari badala ya aliyekuwa Waziri wa nchi za kigeni Mheshimiwa Kalonzo Musyoka. Nchi ya Kenya kwa maoni yangu inakosa uhusiano mwema na jamii ya Kimataifa kutokana na kuyumbayumba kwa Wizara ya nchi za Kigeni. Licha ya Chirau Mwakwere kushtakiwa kuwa na uhusiano wa mahawara jijini Nairobi, Rais Kibaki alimteua Waziri wa nchi za kigeni na kumhamisha Kalonzo Musyoka. Kabla ya ubwabwa kumtoka Mwakwere shingoni amehamishwa na akateuliwa Raphael Tuju. Raphael Tuju ni msemaji hodari; ndio sikatai. Ana elimu hasa tunapoelezwa kwamba aliisomea taaluma ya habari na ni Alumunae wa shule maarufu nchini ya Starehe. Kasoro yake ni kwamba Wakenya walio wengi wanamhusisha na vifo vilivyotokea Mkoani Nyanza. Hali ambayo inamfanya asipendeke hasa miongoni mwa jamii ya Waluo. Ana uwezo wa kuwa Waziri katika Wizara yoyote ile lakini si hii ya kumwakilisha Rais katika nchi za kigeni. Swali ni je Tuju akipewa miaka mingine 5 kama Waziri wa nchi za kigeni atakuwa na umaarufu na uwezo wa kuomba kura na kupewa na Wakenya walio wengi?
ELIMU SIO MUHIMU NCHINI KENYA
Nchini
Kenya elimu si muhimu hata kidogo. Licha ya serikali kutumia fedha nyingi kuwaelimisha wanafunzi, wanafunzi hawa hawapewi nafasi ya kulijenga taifa kulingana na elimu waliyoipata. Hata uwe Professa mwenye digrii milioni moja hamna wa kutambua maarifa uliyo nayo angaa akupe nafasi ulikwamue taifa hili kutokana na tope la umaskini. Mfano ni Wangari Maathai ambaye juzi amepewa tuzo la kimataifa. Ole wake maanake Serikali ya Kibaki haitambui umaarufu wake na anachoweza kupata sasa ni unaibu wa waziri mbali si Uwaziri.
Kuna binti hivi majuzi aliteuliwa kuwa mnaibu wa wizara ya vijana kisha akahamishwa mara moja hadi wizara isiyolingana na elimu yake. Nina uhakika Mbarire angetekeleza majukumu vizuri iwapo angeachwa pale maanake kipawa na elimu yake i pale.
Yashangaza kusikia sekretari aliye na cheti pekee ndiye Waziri wa afya ilahali kuna wabunge jamani waliosomea Utabibu. Maina Kamanda ni naibu wa waziri pia licha kwamba elimu yake imepigiwa maswali. Kalembe ndile ni waziri wa utalii licha kwamba hana uwezo wa kuhamasisha ulimwengu kuhusu uhifadhi wa mazingira. Hata ingawa Prof Kivutha Kibwana ameisomea Sheria na uundaji wa katiba alichoweza kupata katika serikali hii ni uhifadhi wa miti.
Tumearifiwa katika gazeti la Standard kwamba uteuzi wa Mabalozi unategemea unasaba wako na watu maarufu katika serikali. Aliteuliwa kakake Wilfred Machage, Kisha Mwakwere akamteua dadake, balozi mjini
Tokyo ni wa familia ya Moody Awori n.k. Uteuzi wa makatibu wa wizara vilevile si katika misingi ya elimu bali ni jinsi ulivyojiweka katika mtandao. Simeon Nyachae aliwaleta Wakisii kadhaa ambao wana unasaba, naye Musikari Kombo alikuwa ameapa kutokubali Uwaziri iwapo Waluhya hawatapewa nafasi kadha kama wakurugenzi wa mashirika ya serikali.
Kiraitu Murungi alipokuwa Waziri wa Sheria amewaleta Wameru kibao katika wizara hii, swala ambalo huenda likampa kazi maradufu Waziri mpya Martha Karua.
Haikosi hii ndiyo sababu wasomi wengi wasio katika mtandao wametorokea nchi za kigeni kutafuta ajira. Kumbuka wengi wa wasomi hawa walielimishwa kwa mikopo ya serikali na badala ya kupewa nafasi ya kufaidi umma kwa elimu waliyoipata serikali inawaajiri ndugu za mawaziri. Walio na elimu nchini Kenya ndio wanalisukuma taifa kwa kodi wanayotozwa licha ya mishahara
yao kuwa midogo. Mifano ya watu hawa ni walimu. Wasomi tuamkeni tudai haki yetu. Haiwezekani taifa kusonga mbele iwapo halitumii elimu ya raia wake na kuilipia elimu ile ipasavyo.
SEHEMU ZA SIRI ZANYIMWA HAKI MAREKANI.
Haya ndiyo maendeleo wanayojivunia. Ya wanaume kuwa na uhusuano wa kimapenzi na wanaume wenzao. Yashangaza kuwaona wanawake wakikiuka kanuni za kimapenzi; kwamba sharti mwanamke aridhishwe kiu na mwanamume bali sio mwanamke mwenzake. Hii ndiyo demokrasia wanayoizungumzia na kuitangaza kote ulimwenguni. Dhambi ya aina hii imeambukizwa vijana pia huku Marekani na huwezi katu kuwakaripia maanake sheria za nchi zinalinda demokrasia,
kama wanavyosema. Unapotazama filamu zao mojawepo ya maudhui ni ngono za jinsia moja.
Inapotukia ngono kati ya mwanamume na mwanamke, mambo yanakuwa ya firauni sasa. Midomo imechukua nafasi ya sehemu za siri ya mwanamke na mwanamume.Yashangaza kusikia jinsi hawa 'walioendelea' ni wachafu hasa katika midomo
yao. Mbona mwanamke anyonye shakawa za mwanamume huku mwanamume akipata uhondo katiba kukiramba kile kidude. Ikizidi wataziramba ngoko pia; kunakotokea kinyesi. Nimekuwa makini sana kutompa busu yeyote hapa Marekani maanake sijui dakika chache zilzopita alikuwa akifanya kazi gani na siko tayari kupakwa kinyesi katika shavu langu mie.
Kuna msamiati huku kwa jina sherehe za kimapenzi au kwa king'eng'e wanaziita 'sex parties'. Hapa swala kuu si kuonja vyakula mbalimbali vilivyotayarishwa bali ni kumuonja yeyote yule aliyekuja. Hamna faragha hapa. Ngono zitafanywa wazi sakafuni, kutani, vitandani kwenye makochi n.k. Juzi kumekuwa sherehe hapa chuoni Brown. Waliita sherehe
yao 'Gay Students Association'. Ili uweze kukubalika, ulihitajika kuja pale ukiwa uchi au chupi na kanchiri pekee. Nilikuwa pale kushuhudia jinsi 'demokrasia' imekengeusha wanafunzi Wamarekani.
Usimwone binti na ghulamu wamekubatiana ukadhani itakuwa hivi hadi kifo kitakapowatenganisha. Jana binti huyu alikuwa na boifrendi tofauti na juzi na atakuwa tofauti pia ijapo kesho kutwa. Katika ndoa ni vivyo hivyo. Iwapo mwanamume ameanza kulegea basi huenda akaletewa ndume kazi kitandani mwake. Katika matangazo yao utaona tangazo
kama hili;
"Mimi na mume wangu tumeamua kuwa na mhusika wa tatu katika ngono. Ningependa
kumtazama mume wangu akifanya ngono na mwanamke mwingine…."
Mniambie Wakristo nikidhani pia Waislamu, je haya yanakubalika katika dini? Licha kwamba wenzetu hawa ni matajiri wa tekinolojia wao ni maskini hohehahe wa kimaadili. Nina uhakika bara la Afrika ndilo linaongoza ulimwenguNI katika kuwa na utajiri mkubwa wa maadili ya jamii.
WAMAREKANI WANAVYOMTHAMINI MBWA.
Tofauti na wakenya walio wengi, kwa Wamarekani mbwa ni almasi iwapo si dhahabu. Huyu ni kiumbe aishiye kwenye makasri na wanadamu huku Marekani. Akiwa ndani ya kasri basi mbwa huyu ana haki ya kuingia chumba chochote atakacho pasi kubisha hodi. Haijalishi chumba atakamoingia mbwa atampata mwenye nyumba akiwa uchi au la. Waama mbwa wa kiafrika atamwonea gere mbwa wa kimarekani kwa jinsi ambavyo mbwa huyu analelewa kwa utashi.
Ni nadra kumpata mkenya akimpa busu mbwa. Wamarekani swala hili si hoja. Nikidhani mwenye mbwa atampa mbwa wake busu la kukata na shoka kuliko jinsi atampa mpenziye. Kwetu sisi hatuwabusu mbwa mbali tunavitupilia mbali vyombo alivyonusanusa mbwa huyu.
Ukija Marekani ndugu utashuhudia haya bila shaka. Mabwana na mabibi wakiwa ziarani na mbwa wao hawasahau kubeba mikoba ya kuokotea vinyesi vya mbwa. Mwenye mbwa yu macho kutizama mbwa wake atakapochutama. Mara moja atatoka mbio kama mshale kwenda kuokota kinyesi na kukitia mkobani. Eti wanjali mazingira! Kwetu sisi harufu ya kinyesi cha mbwa itaweka makunyugu pua zetu na kutufunga macho kwa ghafla angalau tusikione kinyesi.
Waama mbwa nchini marekani wana bajeti kubwa yakhe! Nina uhakika kiasi cha fedha kitumiwacho kwa mbwa nchini Marekani kila mwaka chatosha kulikwamua bara la Afrika kutoka katika lindi la umaskini. Mbwa atalishwa kwa chakula kilichosawazishwa, atakingwa kutokana na maradhi, atakuwa na yaya wa kumlinda nyumbani miongoni mwa matilaba mengine.
Waliotazama janga la kibunga cha Katrina mtakubaliana nami kwamba ilkuwa heri mbwa kuokolewa kwanza kisha tuanze kutafuta binadamu alipo. Mbwa wengi waliokolewa kutoka vyomba vilivyokuwa vimesombwa huku watu wakifa maji.
Iwapo bwana enda safari na mbwa wake na iwe kwamba atatumia gari basi mbwa atakuwa na kiti chake spesheli. Ole wako mkenya uliozoea kuomba lifti. Samahani maanake kiti kishakaliwa tayari na mbwa! Ukipenda basi jisombe nyuma palipo mizigo na katu usitatize starehe za mbwa wangu. Ikizidi vilevile, usimtamzame mbwa wangu kwa jicho la dharau maanake nitakufungulia mashtaka kortini.
Visa vingi kortini ni vya huyu kamwiba mbwa wangu, yule alimtisha mbwa wangu, huyo hampendi mbwa wangu n.k. Mbwa ni msamiati wa kila mara bongoni mwa Mahakimu na Viongozi wa mashtaka. Mbwa angekuwa na uwezo wa kujitetea angetiwa vizibani kujitetea huku Marekani.
Amini usiamini huku Marekani talaka ni jambo la kawaida. Ndoa huku ni kandarasi. Nikichoshwa na yako mapenzi nenda potelea mbali! Uniache na mbwa wangu. Imekuwa heri kwao kuishi na mbwa kuliko kuishi na libaba lililioshiwa na nguvu za kiume. Nadhani mbwa angekuwa na uwezo wa kufanya mapenzi na binadamu basi ungempata vitandani na wake au waume za watu wakizicheza.
Mambo yalivyo huku ndugu ni kwamba wamarekani wanampa mbwa nafasi ilyovuka mipaka. Ni sawa siwapingi lakini inapofikia kiwango cha kutojali binadamu mwenzako, mpenzio n.k basi nafikiri huku ni kukengeuka. Jumapili baadhi yao hawendi kumwabudu mwenyezi MUNGU aliyewapa hao mbwa. Badala yake huwa ni nafasi nzuri ya kuwatembeza mbwa wao. Mambo Mbotela, unambie leo, huu ni uungwana?
BIASHARA YA ELIMU: TUIGE MAREKANI
Ukweli ni kwamba popote walipo Marekani sharti wawe na lengo la kupata faida. Iwapo sivyo, watafunganya virago na kuondoka. Nchi hii imejiendeleza katika kila hali kwa kuwekeza mtaji katika biashara za kilimwengu. Kila taasisi Marekani imeajiri wataalam wa biashara kwa lengo la kupata maarifa ya jinsi ya kufanya biashara.
Baadhi ya biashara ambazo Marekani wamefanikiwa ni biashara ya uhamiaji, biashara ya shule za kimataifa katika nchi geni, biashara ya mitihani k.v. TOEFL, SAT, GRE , biashara ya kutoa mikopo kwa mataifa maskini n.k. Vyuo vikuu vimechangia pakubwa pia katika kuujenga uchumi wa Marekani.
Katika makala hii nitafafanua jinsi vyuo vikuu vinafanikisha biashara za Wamarekani. Vyuo hivi hutangaza nafasi kwa walimwengu bali sio kwa Wamarekani pekee. Wamefanikiwa kufanya hivi kwa kuweka vyuo hivi vyote katika mtandao kiasi kwamba mwenye kiu ya elimu atapata habari kuvihusu kwa urahisi. Iwapo wewe si Mmarekani utahitajika kufanya mitihani kadha ili uweze kukubalika. Mtihani maarufu ni ni TOEFL ambao haujali iwapo kama ulifunzwa Kiingereza na malkia
Elizabeth mwenyewe. Mitihani hii inaizalishia Marekani mabiliono ya pesa kutoka kote ulimwenguni.
Ukishapasi TOEFL, mambo bado; utahitajika kulipa fedha za usajili chuoni zisizorudishwa. Vyuo vingi vitatoza kati ya Dola 50 na 100. Nitawapa mfano wa chuo kikuu cha Brown. Waliotuma maombi ya usajili mwaka huu walikuwa takribani 17,000. Hawa wametoka sehemu mbalimbali ulimwenguni. Hivyo basi ina maana kwamba chuo kilikusanya shilingi milioni 8,568,000 za
Kenya. Miongoni mwa hawa 17,000 ni 2,400 waliokubaliwa kujiunga na chuo. Hii ina maana kwamba 14,600 hawakubahatika licha kwamba washalipa shilingi 5,040 kila mmoja. Wengi wa hawa wasiokubaliwa ni wa kutoka nchi za kigeni.
Pesa hizi na pamoja na karo inayolipwa na waliofanikiwa, ndizo hutumika kulipa mishahara ya Wahadhiri na wafanyikazi wengine Chuoni. Kwa njia hii vyuo hivi havitegemei kamwe pesa zozote kutoka kwa serikali.
USAWA WA MWANAMKE NA MWANAMUME: MADHARA YAKE
Nchi yetu ya
Kenya imetambulika kukumbatia maswala ibuka ya kilimwengu pasi kupigia maswali madhara yake. Aghalabu badhi ya maswala haya yameibuka katika mataifa ya magharibi kisha yakaenezwa kwa lazima ama kwa hiari katika mataifa yanayoendelea. Mifano ya maswala haya ni Usawa wa kijinsia, demokrasia, kutoadhibiwa kwa mtoto n.k.
Usawa wa kijinsia ni ile hali ya mwanamke kufanywa sawa na mwanamme licha ya tofauti zao za kibaolojia. Katika mhemko huu wa kilimwengu, mwanamke hukakania kudai kwamba chochote awezacho kufanya mwanamume ,mwanamke pia aweza. Labda lililobaki ni mwanamume kutiwa ujauzito na mwanamke. Kwamba kielimu, kifamilia,kisiasa,kidini, kiuchumi, mwanamke anaweza kufanya
kama au bora zaidi ya mwanamume. Katika siasa Ngilu,maathai,Karua,Nyiva,Ndetei,Mugo na wengine wamedhihirishia bara hili na ulimwengu kijumla kwamba mwanamke ni sawa na mwanamume.
Lakini swali ni je usawa huu una madhara yepi kufikia sasa? Nchini Marekani mwanamke amejichukuliwa sawa na mwanamume kiasi ya kwamba atakuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa. Hali hii imepelekea wanawake kuuawa ovyo na waume zao nchini Marekani. Pili ndoa zinavunjika kila wakati Marekani na imekuwa kawaida sasa. Wote ni vichwa katika familia na mwanamke katu hakubali nafasi aliyopewa na dini ya Kikristo kwamba atakuwa msaidizi wa mwanamume. Talaka imekuwa msamiati wa kutamkwa hata na mtoto mchanga Marekani. Hivi sasa idadi ya wanawake waliotalikiana na waume zao Marekani inazidi kuongezeka. Wanawake kama hawa aghalabu huwa hawana nafasi nzuri zaidi ya kujipatia waume wengine maanake wamezeeka. Mwanamume kigogoyo kwa kiasi kikubwa atapata kibinti kirembo hata baada ya kutalikiana na mkewe.
Katika sekta ya uajiri wanawake wamedai nafasi sawa pia. Ukweli ni kwamba hata ofisi iwe na wanawake kiasi gani kuna kazi ambazo watahitaji msaada wa wanaume. Hapa chuoni Brown, sera ya uajiri sawa wa wanawake na wanaume imeleta hasara badala ya faida. Mfano ni ofisi ya usajili amabayo asilimia kubwa ya wafanyikazi ni wanawake. Kazi kama vile za kuinua vitu vizito na kwenda kupokea barua posta imelazimu waajiri wanaume wa muda. Kumbuka ilidhaniwa kwamba wanawake hawa watafanya kazi zote hizi lakini wapi.
Nchini
Kenya wengi wanaojiita watetezi wa haki za mwanamke wametalikiwa na waume zao pia. Sitataja majina kwa usalama wangu na wao. Wanaume ulimwengu mzima wana tabia sawa kwa kiasi kikubwa dada zangu. Hawataki ushindani katika familia. Wanaona fahari kuwa wakurugenzi wa familia zao na kamwe hawatarajii wake zao kujilimbikizia hadhi hii hata wanapokuwa maiti kaburini. Mwanamke anayetazamia mumewe aingie jikoni apike kisha aingie dobi na kufua nguo anajidanganya. Wengi wa watetezi wa haki za mwanamke wamejipata katika visiwa vyao pekee, bila wa kumwita mpenzi karibu. Wengi wameishia mahakamani kushtaki wake wenza kwamba wamewaiba waume zao. Kasoro ni nyie kutaka nafasi za waume zenu.
Watoto wanapokua, wanaanza kudai baba zao. Hawako tayari kujisajili shuleni kwa majina ya mama zao eti David Wambui, au Peter Adhiambo. Swala hili linawapa tumbo joto wanawake waliotalikiwa na waume zao kwa kudai usawa nyumbani. Vitoto vya kike vilivyoambukizwa ugonjwa huu wa usawa wa mwanamke vinaishia kuona ya Firauni. Licha ya wavulana kuwaahidi paradiso hapa duniani, vibinti hivi vinaishia kutumiwa kimapenzi tu kisha waume wasiokubali usawa wanaishia kuoa wanawake wanyenyekevu.
Maswala kama haya miongoni mwa mengine yanastahili kutiliwa maanani na wanawake kabla ya kubugia mihemko ya magharibi kikondoo.
-
Recent
- MAREKANI INAVYOFADHILI VITA BARANI AFRIKA.
- MISHAHARA YA WABUNGE KENYA: WIZI! WIZI! WIZI!
- SIKUKUU YA KUVUTA MARIJUANA MAREKANI.
- UBAKAJI: NJOKI NDUNG’U ANAFICHA HABARI FULANI.
- MADHARA YA KUWEPO SARAFU AINA MOJA AFRIKA MASHARIKI.
- KUNA HATARI YA KALONZO MUSYOKA KUWA RAIS?
- NAMNA YA KUPIMA UBORA WA MAISHA.
- KIFO NI NINI?
- KITOTO CHA MAREKANI KINASAFIRI ULIMWENGUNI ZAIDI YA MHADHIRI CHUONI AFRIKA.
- KUTOJUMULISHA MIKOPO YA WAFADHILI: HEKO SERIKALI
- MBONA MAREKANI NA UINGEREZA ZINAINGIA TANZANIA BILA BREKI?
- KAMUSI YA ISIBATI
-
Links
-
Archives
- May 2006 (2)
- April 2006 (14)
- March 2006 (12)
-
Categories
-
RSS
Entries RSS
Comments RSS